KAMA ulikuwa unadhani klabu ya Yanga inatania katika kesi yao dhidi ya Bernard Morrison basi jua kuwa klabu hiyo ipo siriazi na hiyo ni baada ya Mahakama ya Usuluhishi wa michezo CAS kuweka wazi kuwa utaisikiliza kesi hiyo Alhamisi ya Julai 29,2021.
Hapo awali CAS walitoa taarifa kuwa wangeisikiliza kesi hiyo Julai 23 ambapo baadaye walitoa taarifa kuwa siku ya Eid Al Haji ilisababisha wao kusogeza mbele ambapo juzi Jumamosi kupitia tovuti yao waliweka ratiba ya kesi watakazosikiliza ikiwepo ya ile ya Yanga na Bernard Morrison.
Kupitia tovuti hiyo ya CAS wameorodhesha kesi tatu zitakazosomwa hivi karibuni ambapo kesi namba CAS 2020/a/739 Yanga SC na Bernard Morrison, itasikilizwa Julai 29 huku kesi inayofuatia ikisikilizwa Agosti 5 yenye namba CAS 2021/a/7799 Yeni Malatyaspor na Mitchell Glenn.
Kwa upande wa uongozi wa Yanga, umesema kuwa bado unafuatilia kesi ya winga Bernard Morrison ambaye amehamia Simba, huku wakiweka wazi kuwa wanaamini haki itatendeka,huku wakiamini kuwa Simba watapokonywa ubingwa waliouchukuwa kwa kuwa wamemchezesha mchezaji asiyekuwa halali.
Bernard Morrison kwa sasa anacheza katika klabu ya Simba, ambapo kabla ya kujiunga na klabu hiyo alikuwa akiichezea Yanga, huku usajili wa kuhamia Simba ukigubikwa na utata mkubwa ya kimkataba.
Aidha baada ya Morrison kujiunga na Simba, Yanga waliamua kupeleka kesi hiyo katika mahakama ya usuluhishi CAS ambayo mamlaka hiyo inaendelea kufanyia kazi kesi hiyo.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Afisa Habari wa klabu ya Yanga, Hassani Bumbuli alisema kuwa watu wanatakiwa wawe watulivu kuhusu kesi hiyo kwani bado inafanyiwa kazi na mamlaka husika hivyo baada ya maamuzi watawapora Simba ubingwa wa ligi.
"Haki itatendeka juu ya kesi hii, watu wanaona kama ni utani kuhusu hii kesi ila ipo siku watafahamu kuwa kweli Yanga ilikuwa haitanii,hivyo mashabiki wa Yanga wanatakiwa kuwa wapole kwani hata ubingwa huu waliouchukua Simba tutaupora baada ya kesi kukamilika"alisema kiongozi huyo.