Thursday, June 24, 2021

WAZIRI SIMBACHAWENE AINGILIA KATI MGOGORO WA ARDHI JESHI LA MAGEREZA, WANANCHI CHIHIKWI, MSALATO DODOMA


Na Mwandishi Wetu, MoHA – Dodoma.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewataka wananchi wa Kitongoji cha Chihikwi, Kata ya Mbarawara, jijini Dodoma, wasubiri majibu ya Serikali kuhusu mgogoro wa ardhi kati yao na Jeshi la Magereza.

Mgogoro huo wa ardhi ambao ni wa miaka nane, ulimfanya Waziri Simbachawene kufikia katika Kitongoji hicho na kufanya ukaguzi wa eneo hilo na baadaye alizungumza na wananchi hao ambapo walipewa nafasi ya kutoa maoni na kero zao.

Akizungumza baada ya kuwasikiliza, Waziri Simbachawene alisema ataenda kutafakari na kufanyia kazi malalamiko yote yaliyotolewa na atakrudi kutoa majibu kwa wananchi hao na yatazingatia umuhimu wa pande zote mbili.

Alisema licha ya kuwa anatarajia kuja na majibu ya maoni hayo lakini wananchi hao wanapaswa kujua kuwa ardhi ni mali ya umma, kama serikali inaweza ikaichukua ardhi kwa ajili ya masuala ya umma na wananchi wanapaswa kupisha kufanya shughuli yake na pia haki ya mwananchi kulipwa fidia kwa kile alichokiendeleza katika ardhi na siyo vinginevyo.

"Nimesikia maoni yenu lakini lazima niende nikatafakari, nitahakikisha mimi mwenyewe nitarudi hapa hapa katika mti huu huu kutoa majibu, mapema iwezekanavyo, nafahamu kabisa kamati ya kufuatilia mgogoro huu ilifanya kazi kubwa na mlikuwa na wawakilishi wenu, tufikirie kumaliza huu mgogoro ili shughuli zingine ziendelee," alisema Simbachawene.

Waziri Simbachawene kabla ya kutoa nafasi kuwasilikiza maoni yao wananchi hao, alitoa mipango ya Jeshi la Magereza dhidi ya wananchi hao ambao wanadaiwa walivamia eneo hilo la Magereza, ambapo walitengewa eneo lenye ekari 20 kwa ajili ya kaya 86 ambapo kila kaya watapewa eneo la robo eka ili kuendelea na makazi yao.

Simbachawene ambaye aliambatana na Mbunge wa Jimbo hilo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde katika ziara hiyo, alisema makubaliano hayo yalifanyika kwa maridhiano kati ya Magereza na wananchi wa Kitongoji hicho na waliridhia na Waziri huyo alifika kuzungumza na wananchi hao kwa ajili ya kufanya maamuzi ambayo yataridhiwa na pande zote.

"Ninawashukuru, nafahamu Kamati ilifanya kazi kubwa, kulikuwepo na wawakilishi wenu, maoni ya Mwenyekiti, maoni ya Diwani ebu wote tufikirie jinsi ya kwenda kumaliza mgogoro ili tuendelee na mambo mengine," alisema Simbachawene.

Akizungumzia mgogoro huo, Mkazi wa Kitongoji hicho, Elias Kapugi, aliiomba Serikali kuwafikiria wakati wanataka kuwaondoa katika eneo hilo kwasababu wao wanafamilia na Watoto wamekuwa wakubwa, hivyo kutoa robo eka kwa kila kaya sio sahihi, hivyo wanaomba waliofikisha miaka 18 nao wapewe eneo.

"Hatuwezi kushindana na Serikali, ila tunaomba mambo mawili, moja kuwafikiria hawa waliofikisha miaka 18 nao wapewe ardhi, na pia litengwe eneo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, shule na huduma zingine za kijamii," alisema Kapugi.

Naye Diwani wa Kata ya Mbarawara, Charles Ngambi aliwataka wananchi hao watulie na wasubiri maelekezo ya Serikali ili ije na maamuzi mazuri ambayo yatazingatie pande zote mbili.

Mgogoro huo ambao una muda wa miaka nane kati ya wananchi hao na Jeshi la Magereza, ambapo wananchi wanasema eneo hilo ni haki yao na mpaka wa Magereza upo mbali nao, na wapo hapo tangu enzi za wazazi wao ambao walishafariki, lakini Magereza wanasema wananchi hao wamevamia eneo hilo la Jeshi na wananyaraka ambazo zimethibitishwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA).

Mwisho.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...