Ni maneno yaliyozungumzwa wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa Wilaya ya Njombe ikiongozwa na Mwenyekiti Chama Cha Mapinduzi Wilaya Ndg. Edward Mgaya, ambapo imepongeza kasi na umakini uliopo katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuipongeza Halmashauri kwa kuweza kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.4 kutoka mapato ya ndani pekee kuchangia kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.
Akitoa pongezi hizo Mgaya amesema kuwa Halmashauri imeweza kufanya mambo makubwa katika utekelezaji wa Ilani ya CCM jambo linaloleta imani kwa Wananchi kwa Chama Chao na kuwajengea Heshima.
"Tumeweza kutembelea miradi katika Sekta ya Afya, Elimu na barabara. Lakini katika pita zetu unaona ni kwa jinsi gani Wananchi walivyoandaliwa na wanavyojishughulisha na kilimo cha aina tofauti tofauti. Hii inaonyesha maandalizi makubwa yaliyopo katika kutengeneza misingi ya Kiuchumi kwa Wananchi.Lakini pia nyie mmekwenda mbali zaidi na kuweza kuboresha Sekta ya afya na elimu. Mmejenga Zahanati, Kituo cha Afya Makowo ni kituo kizuri, mmeweza kujenga madarasa ya kutosha katika Shule za Sekondari na Msingi na kuanzisha Shule mpya hii inaonyesha jinsi mlivyo wabunifu, mlivyo na umoja, mnafanya usimamizi na ufuatiliaji katika miradi. Hata akija mgeni hatuna wasiwasi miradi yetu inafurahisha.Niwapongeze sana" Alisema Mgaya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda amesema kuwa Halmashauri imeweka utaratibu wa kupeleka fedha katika maeneo ambayo Wananchi wanakua wameonesha nia kwa kuanzisha mradi na kufikia hatua ya boma ndipo Halmashauri huwapatia fedha kwa ajili ya kufanya ukamilishaji wa mradi husika.Bi Mwenda aliendelea kufafanua kuwa licha ya kuwa mbinu hiyo imepelekea ushindani katika Kata na kuibuka kwa miradi mingi kwenye Halmashauri yapo maeneo ambapo mwamko wa Wananchi kuchangia umekua ni mdogo kulinganisha na maeneo mengine katika Halmashauri.
"Tuna ujenzi wa shule tatu mpya za Msingi. Mjimwema,Kambarage na Magufuli lengo la miradi hii ni kupunguza msongamano wa Wanafunzi katika shule zetu.Halmashauri tumeweza kuchangia kupitia mapato ya ndani, tunawashukuru Wananchi kwa kuweza kutuchangia na Serikali pia imetoa fedha kufanikisha ujenzi wa Shule hizi mpya.
Akitoa ufafanuzi kuhusu uchangiaji wa miradi ya maendeleo Mgaya amesema kuwa kazi ya chama ni kuendeleea kuhamasisha jamii isonge mbele na amewataka Waheshimiwa Madiwani kufanya mikutano ya hadhara na kuwaelimisha Wananchi umuhimu wa kuchangia miradi ya mendeleo kwani hata Taifa lilianza na misingi ya ujamaa na kujitegemea.
Wakizungumza kwa wakati tofauti tofauti baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya CCM Wilaya ya Njombe wamesema kuwa Licha ya Halmashauri kuendelea kuwekeza katika miradi ya Maendeleo na miradi mingi kuwa na thamani ya pesa isiyokuwa na maswali, ni vyema maeneo yenye miradi hiyo ikawekewa mipaka na hati za maeneo hayo ili kuepusha migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe ambaye ni Diwani wa Kata ya Utalingolo Erasto Mpete amesema kuwa Halmashauri itaendelea kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika na amewashukuru Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri kwa jitihada kubwa wanazofanya katika kuwapelekea Wananchi maendeleo na kuhakikisha kuwa yale yote yalioagizwa na kuelekezwa na Kamamti ya Siasa yatakwenda kutekelezwa ipasavyo.
Kamati ya siasa ya Wilaya ya Njombe kwa muda wa siku mbili imefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Halmashauri ya Mji Njombe ambapo jumla ya miradi 16 iliweza kukaguliwa yenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.3 kutoka vyanzo mbalimbali vya fedha ambapo miradi hiyo mingi ikiwa ipo katika hatua mbalimbali za umaliziaji na mingine ikiwa tayari inatumika.
Source