Picha haihusiani na habari hapa chini
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Dodoma inamshikilia Luka Nkini mwenye umri wa miaka 38 Mkazi wa Airport Dodoma kwa tuhuma za kujifanya mganga wa kienyeji huku akiwataka baadhi ya akina mama afanye nao ngono kama sharti la kuwasaidia ambapo amejipatia kiasi cha Sh.Milioni 100 na tano na viwanja viwili.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Sostheness Kibwengo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utendaji wao wa kazi kwa robo ya Januari hadi mwezi Machi Mwaka huu.
Kibwengo amebainisha kuwa mtuhumiwa huyo ametenda kosa hilo kinyume na Sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sura namba 329 marejeo ya mwaka 2019.
Aidha amewataja wahalifu wengine ambao walikuwa wakishirikiana na Mtuhumiwa Nkini kuwa ni Hussein Mvungi(44)mkazi wa Himo Mkoani Kilimanjaro ambaye nae ameshakamatwa na amekiri tuhuma dhidi yake pamoja na Bw. John Gabriel Munuo mkazi wa Sanyajuu Siha huku akimtaka Bwana Munuo kuripoti mara moja kwenye Ofisi za Takukuru ambazo zipo karibu naye kabla ya rungu la Takukuru halijamfikia.
Katika hatua nyingine Kibwengo amesema kuwa wameweza kuokoa zaidi ya Shilingi milioni 900 pamoja na Nyumba moja na kiwanja kimoja ambapo kati ya fedha hizo kiasi cha sh Milioni 214,182,548 ni fedha ambazo zilikuwa haziwasilishwi NSSF na waajiri.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Takukuru ametoa wito kwa wanachi kuwa makini na watu ambao ni matapeli kwani wamekuwa wakijifanya ni Maafisa wa Takukuru wa Mkoa kwakuwapigia simu na kuwataka kwenda Dodoma au kuwatumia fedha na kwamba huo sio utendaji wa TAKUKURU hivyo wasihadaike bali watoe taarifa kwenye ofisi za Takukuru.