Saturday, April 10, 2021

Wavuvi 4 Wafa Maji Mtumbwi Ukizama

 


WAVUVI wanne wamekufa maji na wengine watatu kunusurika kifo baada ya mtumbwi wao kupigwa dhoruba na kuzama wakati wakivua samaki katika Ziwa Victoria, wilayani Bunda mkoani Mara.


Kamanda wa Polisi,  mkoa wa Mara, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Daniel Shilla akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea Aprili 7,mwaka huu.


"Tayari nimepatiwa taarifa hiyo kwamba kuna wavuvi wanne  wamekufa maji usiku Ziwa Victoria wakati wakivua samaki," alisema Kamanda Shilla.


Diwani wa kata ya Neruma, Michael Maungo na Kaimu Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Shinji Shinji walibainisha kuwa kuna wavuvi wanne wamepoteza maisha na kuwataja wavuvi waliokufa maji katika tukio hilo kuwa ni pamoja na Kennedy Lukundo (25) mkazi wa kijiji cha Mwiluluma, Jophuley  Mazigo (19) mkazi wa kijiji cha Kisorya, Zacharia Ruhumbika (17) na Masalu Mafuru (22) wote wakazi wa kijiji cha Kenkombyo wilayani Bunda.


Diwani Maungo alisema kuwa katika mtumbwi huo kulikuwa na wavuvi saba na watatu kati yao walinusurika kifo baada ya kuogelea hadi nchi kavu na kutoa taarifa juu ya tukio hilo.


"Tuna msiba mkubwa katika kata yetu ya Neruma, tumepoteza vijana wetu wanne na katika mtumbwi huo kulikuwa na watu saba, watatu baada ya mtumbwi kupinduka na kuzama waliogelea hadi nchi kavu na ndipo wakatoa taarifa juu ya tukio hilo," alisema diwani Maungo.


Viongozi hao wa kata ya Neruma walisema kuwa baada ya tukio hilo wananchi walifanya jitihada za kuopoa miili ya wavuvi waliopoteza maisha katika tukio hilo na kwamba tayari miili  ya watu watatu iliopolewa na kufanyiwa maziko.


Hili ni tukio la pili kutokea wilayani Bunda kwa kipindi kisichozidi miaka miwili, kwani mwaka jana wavuvi wengine wanne walikufa maji wakati wakivua samaki katika ziwa hilo.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...