Serikali imesema mashimo makubwa yote yaliyotokana na uchimbaji wa madini katika Mikoa ya Mara, Geita na Shinyanga yanapaswa kufukiwa ili kurejeshwa katika hali yake ya awali.
Hayo yamebainishwa na leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Hassan Chande wakati akijibu swali la Mbunge wa Bunda Mhe. Boniface Getere.
Katika swali hilo alitaka kufahamu mikakati ya Serikali ya kufukia mashimo makubwa yaliyosababishwa na ulimaji wa barabara na uchimbaji wa madini hasa katika mikoa hiyo.
Akiendelea kujibu swali hilo Mhe. Chande alisema Sheria ya Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004 inaelekeza maeneo yaliyoharibiwa kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini kurejeshwa katika hali yake awali ikiwemo kufukia mashimo, kupanda miti na kudhibiti taka.
Aidha alisema kuwa wamiliki wa migodi yote wanatakiwa kuweka Hati Fungani (Environmental Performance Bond) kama dhamana ya Usimamizi wa Mazingira katika migodi husika. Pia Sheria ya Madini Sura ya 123 inawataka wamiliki wote wa leseni za uchimbaji madini kuhakikisha uzingatiaji wa utunzaji wa mazingira katika maeneo ya uchimbaji wa madini ikiwemo ufukiaji wa mashimo yatokanayo na shughuli hizo.
Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa kwa upande wa mashimo makubwa yanayotokana na ulimaji wa barabara, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeendelea kuhimiza uzingatiaji wa masuala ya hifadhi ya mazingira wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
"Mikakati mbalimbali imewekwa ili kuzingatia utekelezwaji wa Sheria hizi ikiwemo Serikali kupitia Kamati ya Kitaifa ya Kufuatilia Utekelezaji wa Mipango ya Ufungaji Migodi inahakikisha hatua zote za urejeshwaji wa maeneo ya uchimbaji ikiwemo kufukia mashimo yaliyotokana na shughuli za uchimbaji zinazingatiwa ipasavyo," alifafanua.
Kwa upande mwingine Chande alisema Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika migodi husika mara kwa mara imekuwa ikifanya ufuatiliaji na ukaguzi wa uzingatiaji wa matakwa haya ya kisheria.