MKUU wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, amekemea baadhi ya halmashauri kutumia za mapato ya ndani ya asilimia 10 zinazotengwa kwa ajili ya mikopo ya kundi la walemavu, wanawake na vijana na kuzitaka ziendelee kutenga fedha hizo ili kunufaisha vikundi hivyo.
Alitoa rai hiyo katika makabidhiano ya vifaa na fedha taslimu vyenye thamani ya Sh 245,867,100 kama mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri ya Mji Kibaha kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Ndikilo pia alikabidhi amekabidhi pikipiki 12, bajaji moja, toyo moja, mashine moja ya kutengeneza sabuni na fedha taslimu Sh 177,746,400 kwa vikundi 68.
Alisema utoaji wa mikopo hiyo ni takwa la kisheria na ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2025.
Akieleza hali ya utoaji mikopo na marejesho Mkoani hapo alisema mwaka 2019/20 jumla ya Sh bilioni 2.666 zilitolewa kwa vikundi 672 sawa na asilimia 108 ya fedha zilizopangwa kutolewa na marejesho yalikuwa Sh 645,770,927 sawa na asilimia 54 ya fedha zilizokopeshwa.
"Marejesho haya ni duni, fedha hizi ni za serikali lazima mrejeshe ili Watanzania wengine wanufaike na matunda ya serikali yao," alisema.
Ndikilo alisema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 asilimia 10 zitakazotengwa na halmashauri zote tisa ni Sh 2,124,500,000 hadi Februari 2021 fedha zilizokusanywa ni Sh 1,713,172,068 sawa na asilimia 78.54 ya fedha zilizopangwa, fedha ambazo zimefikishwa kwenye vikundi hadi Februari 2021 ni Sh 1,149,459,447 sawa na asilimia 66.92.