Sunday, April 11, 2021

Mashahidi 18 kutoa ushahidi kesi ya kusafirisha kilo 19 za heroin



Mashahidi 18 na vielelezo zaidi ya sita, vinatarajiwa kutolewa katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kg 19, inayowabili raia watatu wa kigeni kutoka nchi zao Latvia na Nigeria.


Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni raia wawili wa Latvia, Linda Mazure na mpenzi wake Martins Plavins, pamoja na raia wa Nigeria, Henry Ozoemena.



Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao, Mahakama Kuu, Kitengo Cha Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.



Ni baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na washtakiwa hao kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo(Committal Proceeding).



Akisoma maelezo yao, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Kassian Matembele, wakili Mzava amedai, Linda alikamatwa Aprili 17, 2019, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,  Dar es Salaam(JNIA), akisafirisha dawa za kulevya ndani ya mabegi mawili yenye rangi ya udongo na nyeusi.



Amedai akiwa katika  eneo la kuondokea ndege, alipitisha mabegi yake kwenye mashine ya kukagulia mizigo na ndipo mkaguzi alipoyatilia shaka baada ya kuona vitu visivyo vya kawaida kupitia mashine hiyo.



Baada ya mabegi hayo kupita Linda alijitokeza kuyachukua na ndipo mlinzi alipomtaka asubiri na baadaye alitakiwa kufungua mabegi hayo ili yakaguliwe tena.



"Linda alifanya hivyo na kutoa vitu vyote ikiwemo nguo zake kisha mabegi hayo yakiwa matupu yalipitishwa tena katika mashine, na iliendelea kubaini kuwepo vitu vingine na ndio ilipoamriwa mabegi hayo kuchanwa na kukutwa na kiasi hicho cha madawa hayo aina ya heroin," amedai wakili Mzava.



Amedai baada ya hapo Linda alikamatiwa na kuhojiwa na jeshi la polisi.



Mzava ameendelea kudai kuwa, Aprili 19, 2019 alikamatwa Plavins eneo la Kariakoo Dar es Salaam na alikiri kumsafirisha Linda kutoka Lativia kuja Tanzania kuchukua dawa hizo za kulevya na walikuwa wakiishi wote King's Hotel.



Muda mfupi baadae, alikamatwa, Ozoemena na katika mahojiano na jeshi la polisi alikiri kumpatia Linda begi moja lilikuwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kg 15, wakati walipokutana Plavins hotelini.



Mbali shtaka la kusafirisha dawa za kulevya, Ozoemena anakabiliwa na shtaka la kuishi nchini bila kuwa na kubaki kwani aliingia nchini Julai mosi, 2017 na wakati anakamatwa kibali chake cha matembezi kilikuwa kimeisha muda mrefu.



Washtakiwa baada ya kusomewa maelezo yao na ya mashahidi, walikubali majina yao, siku walipofikishwa mahakamani, lakini walikana mashtaka yanayowakabili.



Washtakiwa baada ya kusomewa maelezo hayo, Hakimu Matembele amesema, kesi hiyo ameihamishia Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu uchumini na Makosa ya Rushwa kwa ajili ya usikilizwaji. 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...