Idadi ya vifo kutokana na machafuko ya siku kadhaa katika jimbo la Darfur Magharibi nchini Sudan imepanda hadi watu 50, huku 132 wakijeruhiwa. Serikali imetangaza jana hali ya hatari katika jimbo hilo baada ya siku tatu za makabiliano katika mji mkuu wa El Geneina.
Umoja wa Mataifa ulisema jana kuwa karibu watu 40 waliuawa na 58 wakajeruhiwa. Tukio hilo la umwagaji damu ndilo la karibuni kabisa katika ongezeko la machafuko kwenye jimbo la Darfur tangu kusainiwa kwa makubaliano ya amani mwishoni mwa mwaka jana na kujiondoa kwa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.
Mnamo Januari, karibu watu 129 waliuawa na wengine 108 bado hawana makazi baada ya machafuko kama hayo kuzuka El Geneina kati ya watu wa jamii za Masalit na Waarabu. Wakazi wamesema wanajeshi wa ziada waliokuwa wamepelekwa katika mji huo wengi wao wameondoka.