Msanii wa BongoFleva na filamu hapa nchini Gigy Money ameomba kufunguliwa adhabu yake ya miezi 6 baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kusema Vyombo vya Habari vilivyofungwa vifunguliwe ila wafuate sheria na miongozo ya Serikali.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema hilo baada ya kuwaapisha viongozi wapya leo Aprili 4, Ikulu Dar es Salaam,
"Wizara ya Habari, nasikia kuna Vyombo vya Habari mmevifungia, sijui viji- TV vya mikononi vile 'online', vifungulieni lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, tusiwape mdomo wa kusema tunabinya Uhuru wa Vyombo vya Habari, tusifungie tu kibabe" ameeleza Rais Samia Suluhu Hassan
Baada ya Mhe Samia Suluhu Hassan kusema hivyo msanii Gigy Money ameshea 'comment' yake kwenye mtandao wa Instagram kwa kuandika kuwa "Na mimi nifunguliwe jamani, kazi inaendelea mama".
Gigy Money anatumia adhabu hiyo ya kufungiwa miezi 6 kutojihusisha na masuala ya sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) baada ya kufanya vitendo visivyokuwa vya maadili wakati anatumbuiza stejini.