Wednesday, April 7, 2021

Yanga: Mashabiki endeleeni kuwa na furaha, bado tupo imara


 UONGOZI wa Yanga umewataka mashabiki wake kuendelea kuwa na furaha kwa kuwa bado wapo imara na wanaamini watafanya vizuri kwenye mechi za Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho.

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ipo nafasi ya kwanza na pointi 50 baada ya kucheza mechi 23 inafuatiwa na Simba iliyo nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 20 ina pointi 46.

Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema kuwa hakuna ambacho wamepoteza kwa sasa kwani kila kitu kipo kwenye mipango sahihi.

"Mashabiki wetu wanapaswa kuvimba huko walipo na kutamba kwa kuwa bado tupo imara na tunaongoza ligi hilo lipo wazi.

"Kuwa wanyonge haipendezi kwani tuna wachezaji wazuri ambao wanajua kutimiza majukumu yao, bado kazi ipo na tunaamini kwamba tutafikia malengo yetu bila mashaka yoyote yale," amesema.

Mchezo wao ujao kwenye ligi Yanga ni dhidi ya KMC unatarajiwa kuchezwa Aprili 10, Uwanja wa Mkapa, walipokutana mzunguko wa kwanza ubao wa CCM Kirumba ulisoma KMC 1-2 Yanga.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...