Sunday, March 14, 2021

Mbosso Kuanzisha Lebo Yake Wasafi, Afunguka





BADO upepo unazidi kutikisa ndani ya lebo kubwa ya muziki wa Bongo Fleva, Wasafi Classic Baby (WCB), baada ya Raymond Mwakyusa 'Rayvanny' kuanzisha lebo yake, joto la Mbwana Yusuph Kilungi 'Mbosso' naye kuanzisha lebo yake linatajwa kufukuta, RISASI JUMAMOSI limedokezwa.

 

TAARIFA ZA NDANI

Taarifa za ndani kutoka ndani ya lebo hiyo ni kwamba, tayari taa nyekundu inayoashiria hali ya hatari inawaka kwa Mbosso na siku sio nyingi naye atachomoka ndani ya lebo hiyo na kuanzisha ya kwake kama ilivyokuwa kwa Rayvanny."Unajua Mbosso na Vanny (Rayvanny) ni kama walikuwa lebo moja.

 

Mafanikio yao ndani ya lebo yalikuwa hayatofautiani sana hivyo hapana shaka kwamba naye ni muda wake muafaka wa kuondoka."Tena naona kama amechelewa kwa sababu angeweza kuondoka hata kabla ya Rayvanny. "Unajua kigezo wanachokiangalia pale Wasafi ni nidhamu yako katika kazi.



Mbosso hilo hana tatizo nalo."Amevumilia kwa muda mrefu na hata alipoona mwenzake anatoka hakuwa na kinyongo. Kingine wanachoangalia Wasafi ni jinsi gani unaingiza mkwanja wa kutosha ndani ya lebo sambamba na ukubwa wa jina lako.

"Hilo nalo Mbosso amefanikiwa kwani angalia ngoma zake zinavyotrendi kwenye mitandao ya kijamii hususan YouTube ambao ndio maarufu kwa kuwaingizia pesa wasanii," kilisema chanzo makini.

 

STAILI YA KUONDOKA

Chanzo hicho kilizidi kufunguka kuwa, staili ambayo aliondoka nayo Rayvanny ndiyo itakayotumika hata kwa Mbosso na si kama ile aliyotumia Rajabu Abdul 'Harmonize'."Unajua Harmonize yeye hakupata baraka za wazee. Tayari alishakuwa na tofauti na mabosi sasa hilo ndilo lililomfanya atimke bila ya kupata ile heshima ya kuagwa," kilisema chanzo.

 

TAARIFA NYINGINE

Mbali na chanzo hicho, taarifa nyingine ambazo RISASI JUMAMOSI limezipata zinaeleza kuwa, Mbosso anatarajia kuwa na ofisi kubwa zaidi hata ya Rayvanny na taratibu za maandalizi zimeshaanza."Itakuwa ni ofisi moja kubwa na matata sana. Unajua kila aliyehudumu pale anajua thamani na jinsi ambavyo anapaswa kuwa kama msanii hivyo itakuwa ni kubwa balaa," kilisema chanzo hicho.

 

MBOSSO ANASEMAJE?

RISASI JUMAMOSI lilijaribu kumvutia waya Mbosso ili kumsikia amejiandaaje na safari ya kujitegemea lakini simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa.

 

TUJIKUMBUSHE

Wasafi ndiyo lebo ambayo imekusanya wasanii na kuwafanya wang'ae katika muziki wa Bongo Fleva. Wasanii wanaounda lebo hiyo kama Rayvanny, Mbosso, Lavalava, Zuchu na wengineo, wamejipatia umaarufu mkubwa ndani ya muda mfupi na kuyaona matunda ya sanaa yao.

 

Aliyeanzisha safari ya kujitoa kwenye lebo hiyo alikuwa ni Harmonize ambaye alitangaza kuachana na Wasafi na kuanzisha lebo yake ya Konde Gang.

Alipoondoka alipata 'kashkash' za aina yake kufuatia uongozi kumdai fedha za kuvunja mkataba ndipo aweze kuondoka na kutumia nyimbo alizozalisha akiwa kwenye kruu hilo.

 

Harmonize alilazimika kuuza nyumba zake tatu ili aweze kupata shilingi milioni 500 na ndipo akawa huru kuanza kuzitumia nyimbo hizo katika shoo zake.

 

Baada ya Harmonize kuondoka, aliyekuwa anatajwa kuwa yupo mbioni kuondoka na Rayvanny ambaye kweli jambo hilo lilitimia Jumanne iliyopita ambapo aliibuka na kutangaza lebo yake inayokwenda kwa jina la Next Level Music (NLM).

Tofauti na Harmonize, yeye mabosi zake wote walikuwepo kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo hilo na kumpa baraka tele katika kazi zake na kama hiyo haitoshi, yeye bado anaendelea kuwa memba wa Wasafi muda wote.

 

Alipoondoka Harmonize ilikuwa ngumu sana hata kwa wasanii waliobaki kuonekana wanawasiliana na Harmonize kwani ilikuwa ni rahisi kuonekana ni wasaliti.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...