Kagere awazia makubwa Simba
MSHAMBULIAJI wa Simba Meddie Kagere amesema kwa namna kikosi cha Simba kilivyo msimu huu wanastahili ubingwa kufika mbali zaidi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba inaongoza Kundi A, ikikusanya pointi saba, baada ya kushinda mechi mbili dhidi ya AS Vita na Al Ahly kabla ya kwenda sare ya bila kufungana na Al Merrikh ya Sudan.
Kagere ameeleza kuwa safari hii wana kila sababu ya kutwaa ubingwa wa Afrika kutokana na ubora wa kikosi walichokuwa nacho na mbinu za kocha wao.
"Matokeo yetu tunayoyapata kwenye michuano hii ndio yanaonesha ubora wa Simba, lakini hata mbinu za kocha, utaona michuano iliyopita tulifungwa tena kwa idadi kubwa ya mabao mechi za ugenini, lakini safari hii hadi sasa tumecheza mechi tatu hatujafungwa na tunaongoza kundi," alisema Kagere.
Mshambuliaji huyo alieleza kuwa kwa namna walivyojipanga, anaamini msimu huu watavuka hatua ya makundi na kwenda robo fainali, nusu fainali na kutinga fainali.
Alisema Simba kila mchezaji amekuwa akicheza kwa nguvu kuhakikisha anaipa mafanikio na hiyo inatokana na hamasa wanayoipata kutoka kwa viongozi wao.