Sunday, March 14, 2021

Marufuku Wafungwa kutumika kwa kazi binafsi


Serikali imepiga marufuku wafungwa kutoka Magereza mbalimbali nchini kutumika katika kazi binafsi isipokuwa kwa kufuata utaratibu unaotambulika kisheria.

Marufuku hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Khamis Hamza Chilo wakati wa kikao kilichojumuisha askari polisi kutoka Idara zilizopo chini ya wizara ikiwepo Jeshi la Polisi,Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,Jeshi la Magereza,Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa,kilichofanyika mkoani Singida.

Naibu Waziri Chilo amesema wafungwa wana taratibu zao zinazowaongoza katika mfumo wao mzima wakiwa gerezani huku akiwaagiza wakuu wa magereza yote nchini kufuata taratibu hizo kwani kutofuata taratibu hizo kutapelekea baadhi ya sheria kuvunjwa.

"Kuna taarifa za uhakika kwa wafungwa kutumika katika shughuli binafsi ikiwemo kujenga nyumba za watu binafsi na kulima mashamba ya watu binafsi,nimpongeze Kamishna Jenerali wa Magereza,Suleiman Mzee katika kipindi chake ameanza kuchukua hatua Madhubuti kuhakikisha jeshi linarudi katika misingi yake na sasa tunaona magereza inaendelea kuboreka kila uchwao,sisi kama serikali tunapiga marufuku matumizi binafsi ya wafungwa katika shughuli yoyote binafsi ila kwa kufuata utaratibu" alisema Naibu Waziri Khamis Hamza Chilo

Katika kikao hicho Naibu Waziri Chilo ameyatoa maelekezo mbalimbali ikiwemo tuhuma za rushwa kwa askari wa usalama barabarani, upelelezi wa kesi kuchukua muda mrefu,changamoto ya Vitambulisho vya Taifa na askari wa Jeshi la Zimamoto kuwahi katika matukio ya uokozi.

"Pamoja na kazi nzuri mnayofanya lazima tukae chini kwa Pamoja tujitathmini ili tuweze kuona namna ya kuwasaidia Watanzania,niagize ni marufuku kwa askari yoyote kuchukua rushwa,tunamalizana na madereva barabarani hatuendani nao kwa mujibu wa taratibu na sheria,wengine tunawabambikizia tu kesi makusudi ili waonekane tu wamefanya makosa,kama tumemuona amefanya kosa mpelekeni kunakohusika pia suala la kuwalimbikiza mahabusu katika vituo vya polisi kwa dhana ya kusubiri upelelezi ambao unachukua muda mrefu sio suala nzuri,nawaomba wapelelezi mfanye kazi yenu,ni marufuku kuwarundika mahabusu ndio maana dhamana ikawepo wapeni dhamana kwa kufuata sheria na taratibu" alisema Naibu Waziri Chilo


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...