Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Watu wawili wamefariki dunia baada ya kuangukiwa kifusi cha udongo kwenye machimbo ya kijiji cha Mwime duara namba 11C kata ya Zongomela wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema ajali hiyo imetokea Februari 12,2021 majira ya saa moja kamili asubuhi.
"Wanaume wawili ambao ni Kija Walaga( 25) mkazi wa Mwime na Msonga giti ( 36) mkazi wa Itilima, mkoani Simiyu walifariki dunia baada ya kuangukiwa na kifusi cha udongo kwenye shimo la machimbo ya dhahabu katika kijiji cha Mwime kwenye duara Namba 11C, kata ya Zongomela, tarafa ya Kahama mjini, Wilaya ya Kahama",ameeleza Kamanda Magiligimba
Amesema chanzo ni watu hao kuchimba dhahabu bila tahadhali kwani shimo hilo lilikuwa halitumiki kwa muda kwa sababu ya matengenezo.
Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya Kahama ikisubiri ndugu kwa taratibu za mazishi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga anatoa wito kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu kufuata taratibu/miongozo mbalimbali iliyowekwa na viongozi wao pamoja na kamati za madini juu ya uchimbaji salama katika maeneo yao ili kuepukana na ajali zisizo za lazima.