Polisi nchini Myanmar imewasilisha mashitaka mapya dhidi ya kiongozi aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi, katika hatua ambayo huenda ikafungua njia kwa kiongozi huyo kuendelea kuzuiwa kwa muda usiojulikana bila ya kufikishwa mahakamani na kama sehemu ya mkakati wa mamlaka iliyoingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kuongeza mbinyo.
Kwenye mashitaka hayo mapya, Suu Kyi anashutumiwa kwa kuvunja sheria iliyokuwa inatumika kuwashitaki watu waliokiuka vizuizi vya corona, hii ikiwa ni kulingana na mwanasheria wake Khin Maung Zaw, alipozungumza na waandishi wa habari, baada ya kikao na jaji wa mahakama iliyoko katika mji wa Naypyitaw.
Adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha hadi miaka mitatu jela, lakini kuna wasiwasi kwamba ataendelea kuzuiwa kwa muda usiojulikana, hata bila ya ruhusa ya mahakama kufuatia mabadiliko ya Kanuni ya Adhabu iliyoanzishwa na jeshi wiki iliyopita.
Source