SELEMAN Matola, Kocha Msaidizi wa Simba, amesema kuwa wapinzani wao wote ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa pamoja na Al Ahly wameandaliwa dozi zao pale watakapokutana ndani ya uwanja.
Simba ikiwa inaongoza Kundi A kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kukusanya pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Vita, ina kazi ya kusaka pointi tatu dhidi ya Al Ahly, Uwanja wa Mkapa, Jumanne ijayo.
Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano hiyo, wana kumbukumbu ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Waarabu hao wa Misri walipokutana kwenye mchezo wa hatua ya makundi, msimu wa 2018/19, Uwanja wa Mkapa, Dar, Februari 19, 2019.
Al Ahly watawafuata Simba wakiwa na hasira za kulipa kisasi za kufungwa kwa bao la Meddie Kagere.Akizungumza na Spoti Xtra, Matola alisema kuwa wachezaji wao waliopo wanatambua namna kundi lilivyo pamoja na ushindani jambo litakalowafanya waingie uwanjani kupambana bila kuogopa.
"Kundi lipo wazi kwamba ni gumu, sasa hapo wachezaji mtihani wao ni kufaulu kwa kupata ushindi ndani ya uwanja kwa kila timu ambayo tutakutana nayo bila kujali kwamba ni Al Ahly ama AS Vita, mashabiki watupe sapoti," alisema Matola.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, amesema tayari wana mbinu kali ambayo itawasaidia kupata ushindi kwenye mechi hiyo dhidi ya Al Ahly.
Barbara ameongeza kuwa mbinu ambayo itawapa ushindi katika pambano hilo la Ligi ya Mabingwa Afrika ni kuwafanyia uchambuzi wa kina wapinzani wao kwa kufahamu maeneo dhaifu ambayo yatawapa picha ya namna ya kukabiliana nao. Kazi hiyo inaongozwa na mtaalamu wao, Mzimbabwe, Culvin Mavhunga.
"Kuhusiana na mechi yetu na Al Alhy, kitu kikubwa ambacho tunafanya ni uchambuzi wa wapinzani wetu ambao unatuonesha udhaifu wao.
"Uchambuzi huo ni wa kina na ndiyo maana tumewekeza sana katika kipengele hicho kwani inatupa picha ya kuwafahamu wapinzani wetu na sisi juu ya kikosi chatu kilivyo na sehemu gani ambazo tunaweza kuwafunga," alimaliza Barbara.