Saturday, February 13, 2021

Picha : MVUA YA MAWE NA UPEPO YALETA MAFUKO SHINYANGA MJINI...IBINZAMATA, KITANGIRI WAPATA TABU


Na Kadama Malunde- Malunde 1 blog

Mvua iliyoambatana na mawe iliyonyesha kwa takribani dakika 45 kuanzia saa tisa alasiri leo Jumamosi Februari 13,2021 Mjini Shinyanga imesababisha mafuriko na kukata mawasiliano katika baadhi ya maeneo likiwemo eneo la kutoka Ibinzamata kwenda Kitangiri.

Maeneo mengine yaliyoathirika ni Mtaa wa Viwandani, Mnara wa Voda na maeneo ya masoko ambapo maji yameririka kwa wingi kuingia kwenye nyumba za watu yakiwemo maeneo ya biashara na kusababisha uharibifu wa mali mbalimbali.

Malunde 1 blog imefika katika eneo la vivuko/madaraja ya kutoka Ibinzamata kwenda Kitangiri ambapo wananchi wameonekana wakihangaika kuvuka na wengine wakilalamika vibanda vyao kusombwa na maji.

Wananchi wamesema mafuriko hayo yamesababishwa na miundombinu mibovu ya barabara ambapo kuna madaraja na makalavati madogo yaliyoharibika pamoja na mitaro kuziba hivyo kusababisha maji yashindwe kupita.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila amesema tatizo la mafuriko katika manispaa hiyo linasababishwa na ubovu wa miundombinu ikiwemo mitaro na makalavati ya kupitishia maji akibainisha kuwa maeneo yaliyoathirika zaidi ni maeneo yenye tatizo la mito.

 "Hii Mvua imekuja kwa kasi hatukuitarajia, imenyesha kwa muda mfupi ikiwa imeambatana na upepo na kusababisha maji kufurika na kufunika madaraja na maji kuingia kwenye nyumba za watu",amesema Nkulila.

Wananchi wakivuka kutoka Kitangiri kwenda Ibinzamata na wengine kutoka Ibinzamata kwenda Kitangiri. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...