Saturday, February 13, 2021

Waziri Mkuu Ampongeza CEO Wa Simba Kwa Ubunifu Na Uzalendo


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempongeza Mtendaji Mkuu wa timu ya Simba mwanadada Barbra Gonzalez kwa ubunifu na uzalendo wa hali ya juu kwa kushirikisha Wizara ya Maliasili na Utalii kulitangaza Taifa kupitia jezi wanazozivaa katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika zilizoandikwa VISIT TANZANIA.

Pia, Waziri Mkuu amewapongeza mabingwa wa Soka Tanzania Bara, timu ya Simba kwa kushinda mchezo wake wa kwanza katika hatua ya makundi wakiwa ugenini dhidi ya Klabu ya AS Vita huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Februari 13, 2021) wakati akiahirisha Mkutano wa Pili wa Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma. Amesema kitendo kilichofanywa Mtendaji Mkuu wa timu ya Simba ni cha kizalendo na kinapaswa kuigwa na timu nyingine.

Simba inayoongozwa mwanadada Barbra kama Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, ilifanikiwa kufuzu kuingia hatua ya makundi katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.  Timu nyingine ya Tanzania inayoshiriki mashindano ya kimataifa ni Namungo FC ambayo inashiriki kombe la Shirikisho barani Afrika.

Pia, Waziri Mkuu amempongeza mchambuzi maarufu wa michezo nchini Ali Kamwe, ambaye kupitia ukurasa wake wa instagram, ameeleza vizuri maana ya matumizi ya neno VISIT TANZANIA na namna nchi yetu itakavyonufaika na ubunifu huo.

"Kwa mujibu wa maelezo yake, neno VISIT TANZANIA linakadiriwa kutazamwa na wapenzi wa soka takriban milioni 500 kutoka sehemu mbalimbali duniani. Wapenzi hao wa mpira kupitia vituo vya Televisheni vya Canal Algérie, BeIN Sports, Eurosport, ESPN, Arryadia, GTV ya Ghana, MENA beIN Sports na West Africa Canal+ wameshuhudia mchezo wa jana."

"Kwa lugha nyingine ni kwamba neno 'VISIT TANZANIA' lililopo sehemu ya kifuani mwa jezi ya Klabu ya Simba litaonekana kupitia chaneli hizo kwa kila dakika 90 ambazo Simba itashuka dimbani iwe dhidi ya Al-Ahly (Misri), El-Mereikh (Sudan) au dimba la nyumbani kwa Mkapa (Tanzania). Tutavuta watalii wengi kuifuatilia Nchi yetu."

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Tanzania imeendelea kung'ara pia kwenye medani ya masumbwi, ambapo amewapongeza mabondia Mfaume Mfaume kwa kufanikiwa kutetea ubingwa wa East and Central Africa mwezi Decemba 2020; Bondia Ibrahimu Class Mgendera kwa kushinda Ubingwa wa World Boxing Federation Intercontinental lightweight (WBF).

Vilevile, Waziri Mkuu amewapongeza bondia Tonny Rashidi aliyefanikiwa kutetea mkanda wake wa African Boxing Union (ABU) na bondia Shabani Hamadi JONGO aliyeshinda ubingwa wa WBF International Cruiserweight mwishoni mwa Januari 2021. "Bila kuwasahau Mabondia walioonesha uwezo mkubwa wa kina Hassan Mwakinyo, Twaha Kiduku na Dulla Mbabe ambaye atapanda ulingoni tarehe 26 Februari, 2021."

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...