Tuesday, February 16, 2021

Hukumu ya Shamim, mumewe Machi 31

 


Mahakama Kuu kitengo cha uhujumu uchumi na makosa ya rushwa imepanga Machi 31, 2021 kutoa hukumu ya kesi inayowakabili mfanyabiashara, Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida na mkewe, Shamim Mwasha.


Upande wa mashtaka ulipeleka mahakamani hapo mashahidi sita na vielelezo nane, wakati upande wa utetezi ukipeleka mashahidi watatu.


Shamimu anayemiliki Blog ya 8020 na mumewe Nsembo, wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini gramu 439.70, tukio wanalodaiwa kulitenda  Mei mosi 2019 eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.


Upelelezi kesi ya Shamimu na mumewe wakamilika


Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne Februari 16, 2021 na Jaji  Elinaza Luvanda baada ya shahidi wa tatu wa upande wa utetezi ambaye ni Shamimu kumaliza kutoa ushahidi wake.


"Mahakama hii itatoa hukumu Machi 31, 2021 baada ya mashahidi wa upande wa mashtaka na ule wa utetezi kufungua ushahidi wao," amesema Jaji Luvanda.


Septemba, 2020 wanandoa hao walikutwa na kesi ya kujibu na hivyo kutakiwa  kujitetea mahakamani hapo  baada ya mahakama hiyo kupitia ushahidi wa mashahidi sita na vielelezo nane, vilivyotolewa na upande wa mashtaka.


Awali, wakili wa Serikali Costantine Kakula alidai kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya shahidi wa tatu wa upande wa utetezi kujitetea.


Katika utetezi wake, Shamim alikana tuhuma zinazomkabili mahakamani hapo.


Pia alikana kuwa katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwake makopo yanayodaiwa  kukutwa na dawa za kulevya hayajui.


Mbali na Shamimu kutoa utetezi wake, mashahidi wengine ni mumewe na mtaalamu wa CCTV Camera, Lucas Mbaruku aliyeieleza mahakama hiyo kuwa  CCTV kamera iliyopo katika nyumba ya wanandoa hao hajui imetengenezwa na kampuni gani nchini China.


Mbaruku, amedai  kutokana na kutokujua kampuni iliyotengeneza  imekuwa ngumu kwake kuingiza namba ya siri ili iweze kufunguka.


Alibainisha kuwa yeye ni fundi CCTV kamera tangu mwaka 2004, kwamba na stashahada ya masuala ya kompyuta sayansi aliyoipata mwaka 2002 katika chuo cha Help University, kilichopo nchini Malaysia.


"Kazi yangu kwa sasa ni kufunga CCTV kamera katika maeneo mbalimbali na  nina uzoefu wa miaka 14 katika kazi hii na ofisi yangu ipo Mbezi Beach," alidai  Mbaruku.


Alibainisha kuwa Septemba 4, 2020 alifika mahakamani hapo kwa ajili ya kuiwasha CCTV kamera hiyo lakini kwa bahati mbaya kila alipokuwa anaweka namba za siri iligoma.


"Nilishindwa kuiwasha kwa sababu namba ya siri niliyokuwa nikiweka ilikataa na inaonyesha kuwa neno hilo la siri sio sahihi na kwa sababu sikuifunga mimi hiyo nilishindwa," alidai.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...