Mawaziri wa Afya na Mawaziri wa Fedha kutoka Afrika wanatarajia kukutana na Mkuu wa Shirika la Afya duniani, WHO , kujadili mgawanyo sawa wa chanjo za Covid-19.
''Nitawaambia kuwa tunafanya kila tuwezalo kufanikisha kuanza kwa utoaji chanjo barani Afrika,kuokoa maisha na kurejesha uchumi.
Kinachobakia ni dunia inapaswa itekeleza jukumu lake, amesema Mkuu wa Shirika hilo, Tedros Adhanom Ghebreyesus akizungumza na wanahabari katika mkutano wa siku ya Jumatano.
Hatua hiyo imekuja baada ya rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, kuyasihi mataifa tajiri kutoa dozi za ziada za chanjo kwa nchi zilizo masikini.
Nchi tajiri zilinunua karibu dozi za chanjo ya Covid-19 karibu milioni 800, zinazotosha kuchanja idadi yote ya watu wao kabla ya nchi masikini kuwa na uwezo huo, alisema Dkt Seth Berkley, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la chanjo, Gavi.
''Pia wana dozi nyingine bilioni 1.4 ya dozi nyingine za chanjo. ''Lakini kuhakikisha kuwa nchi masikini zinaanza kutoa chanjo kwa raia wake tunatazamia kuzungumza na nchi tajiri na kuwaomba kuchangia dozi za ziada za chanjo kwa nchi Masikini,'' alisema Dkt Berkley katika mkutano ulioandaliwa na jukwaa la kiuchumi la dunia.
''Ikiwa hilo halitafanikiwa, tutawaambia kuwa tutakuwa tayari kununua kutoka kwao,'' aliongeza. Zaidi ya nchi 45 duniani wameanza kutoa chanjo ya Covid-19.
Barani Afrika, Misri, Morocco, Guinea, Mauritius na Ushelisheli pekee zimeanza kutoa chanjo kwa wahudumu wa afya na wale walio katika hatari ya kuambukizwa Nchi hizo tano zinatumia chanjo iliyotolewa kwao na nchi tajiri zilizo washirika wao.
Pamoja na kuwa chanjo ya Pfizer imeidhinishwa, WHO haijatoa ridhaa ya kusambazwa kwa dawa hiyo kwa nchi za Afrika.