Thursday, January 28, 2021

Bumbuli: Sijaridhika na Hukumu, Nitakata Rufaa



BAADA ya kufungiwa miaka mitatu kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu ndani na nje ya nchi na Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Afisa Habari wa klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa hajaridhishwa na hukumu hiyo na leo Januari 28, 2021, atawasilisha rufaa yake.

 

Kamati hiyo ilimpa adhabu hiyo Bumbuli  baada ya kushindwa kulipa kiasi cha Sh. 5,000,000 kama ilivyoainishwa kwenye hukumu yao iliyotolewa tarehe 28 Septemba 2020,  baada ya kiongozi huyo kukutwa na hatia.

 

Taarifa ya kamati hiyo ya maadili iliyotolerwa jana 27 Januari 2021, imeeleza kuwa adhabu ya kumfungia kiongozi huyo kwa kipindi cha miaka mitatu imetolewa chini ya cha 73(8)(a) cha mwongozo wa maadili ya TFF, toleo la 2013.

 

Akizungumza baada ya adhabu hiyo Bumbuli amesema kuwa hukumu hiyo imeshatoka na wameipokea ila kwa upande wake bado hakuridhika na maamuzi hayo na atakata rufaa ambayo wataiwasilisha leo.

 

"Nyundo imeshuka na tumeshaipokea na tutaijadili na uongozi wa Yanga tujue tunafanyaje, na kiufupi hatukuridhika na hukumu ilivyotoka kama ilivyokuwa ya awali na tutakata rufaa ambayo tutaiwasilisha hii leo," alisema Bumbuli.
 

Aidha Bumbuli aliendelea kusema kuwa hata baada ya kumpa adhabu ya mwanzo hukumu haikueleza kuwa anatakiwa alipe hiyo pesa ndani ya muda gani licha ya kamati kumweleza kuwa rufaa ipo wazi.
 
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...