Saturday, January 2, 2021

Benard Membe Atangaza Kung'atuka ACT- Wazalendo


Aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha ACT Wazalendo, Bernard Membe ametangaza rasmi kujiuzulu uanachama na  nafasi ya mshauri mkuu wa chama hicho.

Amesema kwa sasa, atabakia kuwa mshauri kitaifa na kimataifa wa kushughulikia na kupigia debe masuala ya demokrasia kwa taifa lake.

Hatua ya kujiuzulu ameitangaza kijiji kwao Rondo- Chiponda Mkoani Lindi, nchini Tanzania jana Ijumaa tarehe 01 Januari 2021, wakati akizungumza na DW.

Hata hivyo, hakutoa ufafanuzi zaidi juu ya sababu ya kuchukua maamuzi hayo.

Membe amesema,tayari ameandika barua ya kujiuzulu kwa kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kama utaratibu unavyotaka.

Hata hivyo, waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Tanzania katika utawala wa awamu ya nne ya Jakaya Mrisho Kikwete amesema, kwa sasa ni mapema kubainisha mwelekeo wake unaofuata katika vyama vya siasa.

Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kati ya 2007 hadi 2015 ametangaza uamuzi huo leo akiwa nyumbani kwake kijijini Rondo Chiponda, Wilaya ya Mtama Mkoani Lindi ambapo amesema hajafanya uamuzi huo kwa shinikizo lolote na kwamba kwa sasa atakuwa mshauri wa masuala mbalimbali yanayoihusu nchi ya Tanzania na kupigania demokrasia ya kweli.

Mwanadiplomasia huyo alitangaza kuhamia Chama cha ACT Wazalendo miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2020 baada ya kufukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tarehe 28 Februari 2020 na Kamati Kuu ya chama hicho, kisha uamuzi huo kubarikiwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), tarehe 10 Julai 2020.

Membe alifukuzwa kwa tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya CCM, pamoja na kuonywa mara kadhaa, pasina kubadilika.

Baada ya kuhamia ACT Wazalengo, Membe alitangaza kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.



Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...