Idadi ya watu waliokufa kutokana na mripuko wa bomu la kujitoa muhanga kwenye mji wa Galkayo nchini Somalia imepanda na kufikia 16 baada ya majeruhi kadhaa kuaga dunia usiku wa kuamkia leo.
Katika kisa hicho cha jana Ijumaa, mshambuliaji wa kujitoa muhanga alijilipua kwenye mkutano uliopangwa kuhutubiwa na waziri mkuu wa Somalia Mohammed Hussein Roble.
Duru za usalama zimesema, hapo kabla watu waliokufa walikuwa 6 lakini idadi imeongezeka leo na miongoni mwa waliopoteza maisha ni pamoja na maafisa kadhaa wa jeshi.
Kundi la itikadi kali la al Shabaab, limelidai kuhusika na shambulio hilo na kusema lilikuwa limemlenga waziri mkuu Roble anayefanya ziara kwenye mji huo.
Kwa zaidi ya muongo mmoja, kundi la Al-Shaabab limekuwa likipigana kuingusha serikali kuu ya Somalia ili kuanzisha utawala wake chini ya sheria kali za dini ya kiislamu.
Source