Saturday, December 12, 2020

Wapinzani wageuka lulu Serikali ya Awamu ya Tano


Utawala wa Rais John Magufuli umeonekana kuwa nuru kwa makada wa upinzani waliohamia CCM ama kujiunga na chama hicho baada ya kupata madaraka ya uteule.


Uteuzi wa baraza jipya la mawaziri umeongeza nguvu katika dhana hiyo kwamba wapinzani wamekuwa lulu katika awamu ya tano.


Uchambuzi uliofanywa na Mwananchi katika Baraza la Mawaziri lililoanza kazi rasmi wiki hii, kuna waziri mmoja na manaibu waziri watano ambao walikuwa upinzani kabla ya kuhamia CCM katika wimbi la kwanza la aina yake la wabunge na madiwani kujivua uanachama na kupoteza nyadhifa zao na baadaye kurejeshewa baada ya kuziomba tena walipohamia chama tawala.


Mbali na mawaziri hao, pia wapo makada wawili walioteuliwa kushika nafasi serikalini wakiwa upinzani na baadaye kuhamia CCM.


Hata hivyo, baadhi ya wasomi wamesema Rais ana uwezo wa kumteua mtu yeyote ambaye anadhani anaweza kumsaidia kazi, huku wengine wakisema huo ni mpango wa kudhoofisha vyama vya upinzani.


Miongoni mwa mawaziri walioapishwa Desemba 9, Profesa Kitila Mkumbo, ambaye ni waziri wa nchi, ofisi ya rais- uwekezaji, ndiye pekee aliyetokea upinzani.


Profesa Kitila alijiunga na CCM mwaka 2017, akiwa mshauri na mmoja wa waasisi wa ACT-Wazalendo. Baadaye alitangaza kujiunga na CCM. Aliwahi kuwa Chadema, lakini alifukuzwa mwaka 2013 pamoja na kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.


Hali kama hiyo pia ilikuwa kwa Anna Mghwira, ambaye akiwa mwenyekiti wa ACT-Wazalendo aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, nafasi ambayo ni sawa na ya uwaziri. Akiwa madarakani aliamua kujiunga na CCM.


Wengine walipata uteuzi baada ya kujiunga na CCM ambao ni aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi ambaye sasa ni naibu waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (kazi, vijana na ajira). Katambi alihamia CCM mwaka 2017 na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma.


Aliyekuwa mbunge wa Ukonga kwa tiketi ya Chadema, Mwita Waitara naye alijiunga CCM na kupoteza wadhifa huo, lakini akateuliwa kugombea jimbo hilo na kurudi bungeni. Septemba 2018, aliteuliwa kuwa naibu waziri wa Tamisemi. Sasa ni naibu waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (mazingira na Muungano).


Manaibu waziri wengine waliotokea upinzani ni pamoja na aliyewahi kuwa mbunge wa Siha (Chadema), Dk Godwin Mollel ambaye pia alirudi bungeni Februari 18, 2018 na kuteuliwa kuwa naibu waziri wa afya. nafasi ambayo anaendelea nayo.


Pauline Gekul na David Silinde nao walikuwa wabunge wa Chadema, lakini wakahamia CCM kabla ya kuvunjwa kwa Bunge la 11.


Gekul, ambaye ni mbunge wa Babati, ameteuliwa kuwa naibu waziri wa mifugo, wakati Silinde amekuwa naibu waziri wa Tamisemi.


Pia aliyekuwa mbunge wa Kasulu (NCCR Mageuzi), Moses Mashali alihamia CCM na kuteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, wakati Julius Mtatiro aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya CUF, ni mkuu wa wilaya Tunduru.


Wasemavyo wachambuzi


Wachambuzi waliohojiwa na Mwananchi walikuwa na maoni tofauti kuhusu mwenendo huo mpya katika siasa za Tanzania.


Profesa Abdallah Safari alisema ni jambo la kawaida kwa Rais kuteua mtu anayedhani atamsaidia kazi na kwamba hayo ni mamlaka yake ya kuteua anaowataka.


"Yeye ameona wabunge hao wanafaa, watamsaidia kazi, si jambo baya," alisema Profesa Safari ambaye pia ni kada wa Chadema na wakili wa kujitegemea.


Lakini Profesa Safari alisema kuteua makada wanaotoka upinzani kuwa mawaziri au kushika nafasi nyingine kubwa serikalini hakuwezi kuua au kudhoofisha upinzani kwa kuwa wanaoteuliwa ni wachache.


Alisema upinzani utaendelea kuwepo licha ya kupita katika kipindi kigumu.


Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema kuteuliwa kwa makada hao kunaweza kusababisha chuki ndani ya CCM kwa sababu makada waliojitoa kwa muda mrefu ndani ya chama hicho wataona hawathaminiwi.


"Hayo ni mafanikio kwa wale walioteuliwa. Hata hivyo, ndani ya CCM kuna watu wenye manung'uniko, kwa nini wenzao wanaingia na kuteuliwa kwenye nafasi za juu," alisema mwanazuoni huyo.


Lakini Profesa Mohamed Bakari wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema lengo kuu la uteuzi huo ni kuvidhoofisha vyama vya upinzani kwa kuchukua makada wake wenye uwezo.


Profesa Bakari alisema suala siyo vyama vya upinzani kuzalisha makada wazuri au kwamba CCM hakuna makada wenye sifa ya kuteuliwa.


"CCM ina rasilimali kubwa sana ya makada wenye uwezo. Sidhani kwamba ndani ya chama hicho kuna upungufu wa watu wa kushika nyadhifa," alisema.


"Ukiangalia kinyang'anyiro cha kutafuta wagombea, kuna idadi kubwa ya wasomi wanaotaka kugombea au wanaotaka kuteuliwa wanakimbilia chama tawala. Kwa hiyo, si kwamba chama hicho kina makada wachache,'' alisema.


"Ni mkakati wa kuonyesha kuwa ndani ya upinzani hakuna fursa na kwa hiyo wakijipeleka CCM wanaweza kupata fursa pia."

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...