Na Ahmad Mmow, Lindi.
Katika kukabiliana na uharibifu wa miundo mbinu ya barabara na wizi wa alama za usalama barabarani, Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini(TARURA) halmashauri ya manispaa ya Lindi inaanda njia rahisi ya kuwakamata waharibifu wa miundo mbinu ya barabara na wezi wa alama za usalama barabarani.
Hayo yameelezwa na meneja wa TARURA wa halmashauri ya manispaa ya Lindi, mhandisi Lusekelo Mwakyami wakati wa kikao baina ya watumishi wa TARURA wa halmashauri ya manispaa ya Lindi na Mbunge wa jimbo la Lindi, Hamida Abdallah ambaye alitembelea Ofisi ya Wakala huo zilizopo mjini Lindi.
Mhandisi Mwakyami alisema miongoni mwa changamoto ni uharibifu wa miundo mbinu na wizi wa alama za usalama barabarani. Kwahiyo taasisi hiyo inaanda njia za kuwakamata wezi na waharibifu wanaotenda vitendo hivyo ambavyo vinasababisha hasara kwa serikali.
Alisema uchafuzi wa barabara na mifereji ya kupitishia maji ya mvua unaofanywa na baadhi ya wananchi kwenye mitaa na maeneo ya biashara vinasababisha baadhi ya miundo mbinu ya barabara kushindwa kupitisha viwango vya maji vinavyokusudiwa.
" Wizi wa alama za barabarani unaofanywa na baadhi ya wananchi mitaani na uharibifu wa barabara katika baadhi ya mitaa kwakuzoa mchanga kwa ajili ya shughuli za ujenzi ni changamoto kubwa. Sasa hili kuthibiti hali hiyo tuna andaa njia ambayo itawezesha wakamatwe kirahisi bila wenyewe kutarajia," Mwakyami alisisitiza.
Aidha mhandisi Mwakyami alitaja changamoto nyingine kuwa ni uwepo wa miundo mbinu ya maji, umeme na simu iliyojengwa ndani ya hifadhi ya barabarana ambayo inakatiza barabara,ujenzi na shughuli za biashara kwenye hifadhi ya barabara. Hali ambayo inasababisha kuchelewesha kutekeleza miradi kwa muda muhafaka.
" Ujenzi wa miundo mbinu ya huduma nyingine unasababisha TARURA na ULGSP kutumia fedha nyingi kugharamia uhamishaji wa miuondombinu hiyo mara kwa mara pindi matengenezo ya barabara yanapofanyika," alibainisha Mwakyami.
Lakini licha ya njia hiyo inayo andaliwa ili kuwakamata waharibifu na wezi hao, lakini pia Mwakyami alisema TARURA inaandaa utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi. Ikiwemo kuhusu sheria namba 13 ya mwaka 2007 ambayo inadhibiti uharibifu wa barabara na samani zake.
Mbali na hayo mhandisi Mwakyami alisema taasisi hiyo inatarajia kuanza kufanyia matengenezo kwa baadhi ya barabara za kiwango cha lami kwa kutumia miongozo mipya yenye gharama nafuu inayoepusha matumizi ya vifaa vya ujenzi vinavyopatikana mbali na kwa gharama kubwa.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Lindi, Hamida Abdallah ambaye katika mazungumzo hayo aliiomba TARURA ifanyie matengenezo maeneo korofi ya baadhi ya barabara zilizopo katika jimbo hilo alitoa wito kwa taasisi hiyo itumie kikamilifu sheria ili kudhibiti uharibifu wa miundo mbinu na wizi wa alama za barabarani.
Alisema ni jambo lisilokubalika kusikia na kuona miundo mbinu ambayo inatumia fedha nyingi kujenga inaharibiwa mara kwa mara na kusababisha kurudia matengenezo. Kwani fedha zinazozutumika kwa matengenezo hayo zingeweza kutumika kwa ujenzi wa barabara nyingine.
Source