Wednesday, December 16, 2020

DK. GWAJIMA AONGOZA KUAGA MIILI YA WATU 15 WALIOFARIKI DUNIA KWENYE AJALI SINGIDA

 

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk.Doroth Gwajima (wa pili kulia akiangalia eneo ilipotokea ajali hiyo. Kulia ni Dk.Suleiman Muttani wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk.Doroth Gwajima (mbele) akitoa heshima za mwisho mbele ya majeneza yenye miili ya watu 15 waliofariki dunia baada ya Hiace waliokuwa wakisafiria kutoka Mwanza kwenda Itigi kwenye harusi kugongana uso kwa uso na lori la mafuta Kijiji cha Mkiwa mkoani Singida. Miili mitatu kati ya hiyo ni abiria walioomba msaada kutokea Ikungi kwenda Manyoni kwa shughuli za msiba.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk.Doroth Gwajima, (katikati) akimfariji Heri Mkama manusura wa ajali iliyosababishwa na basi dogo la abiria (Hiace) baada ya kugongana uso kwa uso na lori la mafuta eneo la Kijiji cha Mkiwa mkoani Singida. Mkama ambaye ni Bwana harusi mtarajiwa alipata ajali hiyo wakati akiwa na ndugu zake 13 waliokuwa wakimsindikiza kutoka Mwanza kwenda Itigi kwa ajili ya kuoa, hata hivyo kati ya ndugu hao 12 walipoteza maisha kupitia ajali hiyo. 

Dkt.Suleiman Muttani wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida akimuelekeza jambo Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt.Doroth Gwajima wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuwafariji majeruhi wa ajali hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, alitoa salamu za pole na faraja kutoka kwa Rais John Magufuli kwa wote walioguswa na msiba huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akitoa salamu za rambirambi wakati wa kuaga miili hiyo.

Mmoja wa wafiwa wa ajali hiyo akitoa shukurani kwa Serikali na wananchi kwa msaada waliotoa wakati wa ajali hiyo.
Makatibu Tawala wa Mkoa wa Singida wakiwa katika shughuli ya kuaga miili hiyo. Kutoka kushoto ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Deogratius Yinza,, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Winfrida Funto na Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida, Hassan Ngoma.
Katibu wa Barraza Kuu la Waislam 4anzania (BAKWATA) Sheikh Buruan Mlau akitoa salamu za rambirambi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ASP) Sweetbert Njewike akielezea ajali hiyo na hatua zilizochukuliwa na jeshi la polisi.
Mchungaji Michael Mgandila wa Kanisa la Moravian akiomba wakati wa kuaga miili hiyo.
Sheikh wa Wilaya ya Singida, Iddi Simba akiomba dua wakati wa kuaga miili hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskas Mulagiri akielezea utaratibu wakati wa kuaga miili hiyo.

Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima, ameongoza kuaga miili ya watu 15 waliofariki dunia kutokana na ajali mbaya iliyosababishwa na basi dogo la abiria (hiace) kugongana uso kwa uso na lori la mafuta eneo la kijiji cha Mkiwa, wilaya ya Ikungi, mkoani hapa juzi.

Akizungumzia chanzo cha ajali hiyo, mbele ya Waziri wa Afya, Kamanda wa Polisi mkoani hapa Sweetbert Njewike, alisema mnamo Machi 13 mwaka huu, majira ya saa 9.30 alasiri, ndipo ajali hiyo ilitokea kwa kuhusisha basi dogo la abiria lililokuwa likitokea Mwanza kugongana uso kwa uso na lori la mafuta lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenye maeneo yaliyotajwa.

Njewike alisema basi hilo kutoka Mwanza lilikuwa na abiria 14 wanaosemekana kuwa walikuwa wakimsindikiza ndugu yao ambaye ni bwana harusi mtarajiwa kwenda kufunga ndoa na lilipofika eneo la Ikungi mkoani Singida likaongeza abiria wengine 3 ambao waliomba msaada kwenda msibani eneo la uelekeo wa gari hilo, na kufikisha idadi ya abiria 17.

Alisema baada ya kufika kijiji cha Mkiwa ndipo lilipopata ajali hiyo-na abiria 13 walipoteza maisha pale pale, huku majeruhi wengine 2 nao wakifariki kwa nyakati tofauti wakati wakipatiwa matibabu hospitali-idadi iliyofikisha jumla ya vifo 15 vilivyotokana na ajali hiyo mpaka sasa.

"Kwa sasa majeruhi wawili waliotambuliwa kwa majina ya Hema Mkama (Bwana Harusi mtarajiwa aliyekuwa akisindikizwa kwenda kuoa) na mwingine Shakira Hamis wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya St. Gasper iliyopo Itigi, Manyoni," alieleza Njewike.

Aidha, aliwataja waliofariki kuwa ni Mrisho Swedi (Mabatini Mwanza), Swalala Ibrahimu (Mabatini Mwanza), Zakia Ibrahimu (Mwanza), Lamlati Mkama (Mabatini Mwanza), Rehema Hussein (Mabatini Mwanza), Abdul Mirambo (Mabatini Mwanza) na Christian Sande (Mabatini Mwanza).

Wengine ni Halima Rashida (Mabatini Mwanza), Lukuman Ibrahimu (Mabatini Mwanza), Joseph Ludovick (Damankia Ikungi), William Churi (Damankia Ikungi), Anna Gabriel (Damankia Ikungi), Anjela Phinias, aliyekuwa dereva wa hiace hiyo Majaliwa Paschal, na mwingine aliyetambuliwa kama Mama Mdogo.

Gwajima, kabla ya kuongoza kuaga miili ya marehemu eneo la hospitali ya mkoa mapema jana, alianza kwa kutembelea hospitali ya St. Gasper iliyopo halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni, kwa lengo la kuwafariji manusura wawili wa ajali hiyo Heri Mkama (bwana harusi mtarajiwa) na Shakira Hamis.

Aidha, alipata nafasi ya kutembelea eneo la tukio ambalo ajali hiyo ilitokea, na baadaye alitembelea hospitali kadhaa za mkoa wa Singida, ikiwemo ya Rufaa Mandewa na hospitali ya mkoa ili kuhakiki na kujiridhisha juu ya mfumo mzima wa huduma za kitiba pindi ajali zinapotokea.

Akizungumza wakati wa tukio la kuaga miili hiyo, Gwajima pamoja na kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliokusanyika eneo hilo, alionyesha kufarijika na salamu na kiitikio ambacho viongozi wa dini na serikali mkoani hapa wakati wote walikitumia kama kauli mbiu-yaani "Upendo na Amani" kiitikio "Dini Mbalimbali" na kinyume chake "Dini Mbalimbali " kiitikio "Upendo na Amani."

Alisema salamu hiyo ni ishara ya umoja na mshikamano, ni ishara ya upendo na uzalendo, na kiashiria cha ustawi wa maendeleo yanayotokana na mshikamano wa dhati, uliosheheni kiu ya kufikia malengo kama mkoa na taifa kwa pamoja bila kubaguana kwa namna yoyote inayotokana na itikadi za kidini.

Aidha, Gwajima aliwashukuru wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine, katika kuhakikisha wanaokoa maisha ya majeruhi waliotokana na ajali hiyo lakini pia kwa kuwasitiri wengine waliotangulia mbele za haki

"Nimeona nije hapa sababu toka tu pale ajali ilipotokea mfumo wa afya uliingia katikati. Hivyo nimekuja kuhakiki mfumo mzima na kujiridhisha-na ukweli watendaji wa afya wanajitahidi sana kuokoa maisha ya majeruhi waliopo na kuendelea kuwasitiri wote waliotangulia mbele ya haki," alisema.

Aliwataka watanzania kuhakikisha wanafuata sheria za barabarani zilizopo, sambamba na kuunga mkono juhudi za maksudi zinazofanywa na majeshi yetu, hususani maelekezo ya mara kwa mara yanayotolewa na kikosi cha usalama barabarani ili kwa pamoja kuweza kutokomeza matukio ya ajali.

"Kwa upande wa serikali kupitia sisi sekta ya afya tunajitahidi kuelekeza rasilimali tunazopewa katika kuboresha miundombinu ya kukabiliana kikamilifu pindi ajali zinapojitokeza. Na kuna mradi unakuja ambao utakwenda kuimarisha miundombinu yetu kuwa imara na ya kisasa zaidi," alisema Gwajima.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, alitoa salamu za pole na faraja kutoka kwa Rais John Magufuli kwa wote walioguswa na msiba huo.

"Rais John Magufuli ameniagiza kutoa salamu za pole kwa wafiwa, ndugu, jamaa na marafiki na wote walioguswa na msiba huu, anaungana na familia zote katika kipindi hiki kigumu. Mwenyezi Mungu awape uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki-marehemu wote wapumzike kwa amani," alisema Nchimbi kwa niaba ya Rais

Aidha, akieleza utaratibu wa kusafirisha miili hiyo kuifikisha mahali inapotakiwa, alisema serikali itagharamia kila kitu katika kuhakikisha wote waliofariki kupitia ajali hiyo wanasafirishwa na kupumzishwa kwenye makao yao ya milele.

Imeelezwa, taratibu zote za kusafirisha miili hiyo zimekamilika, na kwamba miongoni mwa waliofariki miili 11 itaelekea Mwanza, mwili mmoja utasafirishwa kwenda Mbeya, na miili 3 itaelekea Ikungi kwa taratibu nyingine za maziko.

Kupitia ajali hiyo, mama mdogo wa ndugu hao amejikuta akipoteza watoto wawili, wajukuu wanne, na kitukuu kimoja-yaani watu 7 kwa mara moja ndani ya familia moja, huku Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Singida Dk .Victorina Ludovick naye akijikuta akipoteza ndugu 3 wa familia moja-ambao walipanda basi hiyo kutokea Ikungi.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...