NA THABIT MADAI,PEMBA.
WANAWAKE wanaojishughulisha na ukulima wa mwani nchini, wametakiwa kuwashajiisha watoto na ndugu zao wa kiume kulima zao hilo ili kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.
Akizungumza kando ya mafunzo ya wakufunzi wa wakulima wa mwani yanayoendelea kwenye ukumbi wa makonyo Wawi Mkoa wa Kusini Pemba, Waziri mstaafu wa iliyokuwa Wizara ya Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali, amesema si busara kukiona kilimo hicho kuwa ni kwa ajili ya wanawake peke yao.
Ameeleza kuwa, kilimo cha mwani kina faida kubwa endapo kitaendeshwa kitaalamu, na pia kina nafasi kubwa ya kubadilisha maisha ya wananchi wakiwemo wanaume na kuinua pato la taifa.
Aidha, amewaomba akinamama wanaolima mwani, wawahamasishe watoto wao wa kiume kujiunga na mafunzo ya kilimo hicho, badala ya kuendekeza baraza zisizokuwa na tija.
Balozi Amina amesema iwapo wanaume watachangamkia kilimo cha mwani, wataweza kuchukua nafasi za wazazi wao ambao utafika wakati hawatakuwa na nguvu za kuendesha shughuli za kiuzalishaji na uchumi kwa jumla.
Amefahamisha kuwa, wakati Serikali ya Mapinduzi Zanzibar awamu ya nane ikija na mkakati wa kuimarisha uchumi wa buluu, ni wajibu kwa wananchi wote kuiunga mkono kwa kushiriki kwa vitendo kwenye uzalishaji wa rasilimali zitokanazo na bahari.
Kwa upande wao, wakufunzi 30 wanaoshiriki mafunzo hayo kutoka maeneo mbalimbali ya kisiwa cha Pemba, wameishukuru taasisi ya REPOA iliyoandaa warsha hiyo, wakisema fursa hiyo itawapa mbinu za kitaalamu za kulima mwani katika maji ya kina kirefu sambamba na kuzalisha kwa wingi na kiwango bora kinachokubalika kwenye soko la kimataifa.
Mapema, Mtafiti Mkuu wa REPOA Steven Mombela, amesema taasisi hiyo imebaini changamoto kadhaa zinazowakabili wakulima wa mwani nchini, hivyo wamejidhatiti kuleta mapinduzi kwa kuwaendeleza wakulima wa zao hilo kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kuwapa njia sahihi za kuimarisha ubora.
Mafunzo hayo yaliyofunguliwa Disemba 14, 2020 na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo Soud Nahoda Hassan, yanatarajiwa kufungwa Jumapili ya Disemba 21, mwaka huu.