Tuesday, December 29, 2020

Bobi Wine kurejelea kampeni baada ya mauaji ya mlinzi wake na waandishi habari kujeruhiwa

Mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha NUP Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ametangaza kuendelea na kampeni zake hapo kesho alizokuwa amesitisha kwa siku 3 baada ya waandishi habari 3 kujeruhiwa na mlinzi wake kugongwa na gari.

Kulingana na mwandishi wa BBC Swahili mjini Kampala, Issaac Mumena, siku ya Jumapili Robert Kyagulanyi mgombea kupitia chama cha NUP alisitisha kampeni zake wilayani Masaka, kusini magharibi mwa Uganda baada ya mwandishi habari Ashirafu Kasirye kujeruhiwa vibaya na walinda usalama na kukimbizwa mjini Kampala kupata matibabu huku hali yake ikiwa mahututi.

Akiwa njiani kuelekea mjini Kampala mlinzi wake naye aligongwa na gari ambalo Bobi Wine anadai lilikuwa la jeshi la UPDF na kufariki dunia na mazishi yake yalifanyika hapo jana.

Katika mkutano na waandishi habari uliofanyika leo makao makuu ya chama cha NUP Kamokya kitongoji cha jiji la Kampala Bobi Wine ametangaza kurejea kwenye kampeni kesho akianzia kisiwani Kalanga na baadaye Wakiso hadi jiji la Kampala ikiwa ni kati ya wilaya 13 zilizopigwa maarufuku kufanya kampeni na tume ya uchaguzi kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Covid-19 lakini Bobi Wine amekaidi agizo la tume ya uchuguzi.

''Baada ya kutumia tume ya uchaguzi wamepiga maarufu kampeni zetu sehemu hizo zote, jana nimemuona rais Museveni akiwa Mukono, na nikajiuliza viongozi wa tume ya uchaguzi wanavyofanya kazi zao. Hata hivyo mimi nitafanya kampeni hata kama wamepiga marufuku sehemu hizo nitakuja na kuzungumuza na nyinyi'', amesema Bobi Wine.

Wakati huohuo, Rais Yoweri Museveni anayetetea kiti chake amewajibu viongozi wa kidini kuhusu zoezi la uchaguzi kufanyika kama lilivyopangwa tarehe 14 Januari hata kama kuna virusi vya corona.

Mgombea huyo wa chama tawala cha NRM alitakiwa kufanya kampeni wilaya ya Kampala na Wakiso lakini kwasababu ya marufuku ya tume ya uchaguzi, alizinduwa barabara ya Mukono katosi na kuzinduwa kiwanda cha gesi wilayani Mukono na baadaye kuwahutubia wafuasi wake kwa njia ya telivisoni na radio.

Katika hotuba yake Rais Museveni amesema uchaguzi mkuu hauwezi kuahirishwa kama walivyoomba viogozi wa madhehebu ya Wakristo nchini humo.

''Siyo muhimu tunaweza kufanya zoezi la uchaguzi hata kama kuna virusi vya corona, mtu anakwenda anapiga kura na kuondoka, pia tayari kuna wabunge karibu 13 wamepita bila kupingwa sasa utawezaje kusitisha uchaguzi. Na fedha ambazo zimeshatumika katika zoezi hili na tume ya uchaguzi utazipata wapi, fedha ambazo zimetumika zinaweza kujenga barabara kama tano'', Museveni amesema.

Wagombea wengine wameendelea na kampeni zao kama vile Jenerali Mugisha Muntu ambaye amezungumuza na wafasi wake wilayani Mitiyana kusini magharibi mwa Kampala na kuwaomba kujitokeza kwa wingi tarehe 14 Januari ili wampumzishe Rais Museveni.

''Nchi jirani za Kenya na Tanzania tumeona marais wanapokezana kwa amani kama tulivyomuona Moi akimpatia Kibaki na Kibaki akampatia Uhuru. Tumeshuhudia nchini Tanzania mara nne, ni sharti kutibu ugonjwa huo. Tunawaomba tarehe 14 Januari, 2021, mumpumzishe Jenerali Museveni kwa kura zenu ili aende akapumzike'', amesema Mugisaha Muntu.

Patrick Amuriat Oboi wa chama cha FDC baada ya kupuliziwa maji ya pilipili jana na walinda usalama na kupelekwa hospitali kupata matibabu, amerejea tena katika kampeni akiwa mkoa wa Teso wilaya Bukedea.

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...