WAKATI wanamuziki wa Dansi nchini wanalia njaa kutokana na kile wanachodai muziki wao kukosa soko, shilingi imegeuka upande wa pili.
Msanii Nasibu Abdul 'Diamond Platnumz' au 'Mondi' anapiga pesa kupitia kibao chake cha Waah alichomshirikisha mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Antoine Christophe Agbepa Mumba 'Koffi Olomide' au 'Papaa Mokonzi Le Grand Mopao'.
Ukiusikiliza Wimbo wa Waah hautofautiani sana na midundo ya Bendi ya The African Stars 'Twanga Pepeta' ambayo leo hii imeishia kufanya maonesho ya bure kwenye baa.
Kwa kimbunga cha Waah kinavyozidi kutikisa anga la muziki, unaweza kumuita Diamond afanye shoo ya bure kwenye baa yako inayoingiwa na watu ishirini na mbili?
Jibu HAIWEZEKANI! Lakini je, kuna muujiza wowote ndani ya Wimbo wa Waah ambao umeandika historia kwenye maisha ya Mondi kwa kuwa wimbo wake wa kwanza kutazamwa na watu zaidi ya milioni mbili ndani ya siku moja?
Jibu pia ni HAKUNA; kwa sababu kilichofanyika kwenye wimbo huo, Twanga Pepeta, FM Academia, Akudo Impact, Malaika na bendi nyingi nchini wanaweza kukifanya na kupata matokeo.
Tatizo ni nini? Wanamuziki wa dansi nchini hawataki kuingia darasani kujifunza, hawataki kubadili mfumo wao wa kuburudisha ili kuendana na matakwa ya dunia ya sasa.
Wengi wao wamebaki kutumia staili ileile ya kutunga nyimbo ndefu zilizojaa mashairi ya kuwatukuza mapedeshee ambao siku hizi nao wamekufa kifo cha mende.
Mara nyingi nimekuwa nikisikia baadhi ya wanamuziki wa dansi wakilia kutengwa na vyombo vya habari kwamba haviwapi ushirikiano wa kupiga nyimbo zao.
HOJA; ni nani aliyeanzisha chombo cha habari kuwaboa wasikilizaji wake na kwamba awe tayari kupiga nyimbo ambazo haziwafurahishi watazamaji wa runinga yake?
Jibu ni kwamba; vyombo vyote vya habari vinatembelea nyota ya jamii. Bidhaa ambayo jamii inaihitaji kwa maana ya muziki mzuri ndiyo itakayotolewa na vyombo vya habari.
Kwa msingi huo, kabla wanamuziki na bendi za dansi kulaumu vyombo vya habari vinapaswa kujiuliza vyenyewe; "Vinatoa bidhaa inayopendwa kwenye jamii?"
Majibu lazima yatakuwa mawili; moja ni NDIYO na jingine ni HAPANA; lakini ukweli unabaki kuwa ni HAPANA kwa sababu kama nilivyosema vyombo vya habari havimchagulii msikilizaji nyimbo, bali ni yeye ndiye anayevichagulia vyombo vya habari nini cha kupiga.
Ukiona kazi yako haipigwi redioni, jua hilo siyo chagua la wasikilizaji na wala si kwa sababu hukumpa DJ pesa za kumtongoza akupigie wimbo wako.
Zama hizo zimepitwa na wakati siku hizi kizuri kinajiuza na ukiwazingua wasikilizaji nao wanakuzingua kwa kuhamishia usikivu wao kwenye chombo kingine cha habari.
Pengine niulize wakati Diamond anatoa wimbo wake wa Waah aliwaita wandishi na kuwapa 'bahasha' kwamba sasa nendeni mkanifanye kazi yenu ili muziki wangu usikike?
Alipita kwenye vituo vya waendesha bodaboda na kuwajazia mafuta ili wapige wimbo wake?
Jibu ni HAPANA; kila kitu kinakuja kama upepo wa kisulisuli; mwandishi, sijui prodyuza atakayejaribu kushindana nao atanyakuliwa mzimamzima.
Nini ninachotaka kusema kwa wanamuziki wa Dansi nchini? "Ingieni darasani" mjifunze ni nini Dunia ya leo inataka na hasa kupitia Ngoma ya Waah.
Maana ni wazi kwamba wandishi na watangazaji wa leo wengi ni vijana ambao ni vigumu kwao kuwaza kupiga Wimbo wa Mtu Pesa wa Twanga Pepeta ya zamani kwenye kipindi chake na kuacha kupiga Wimbo wa Litawachoma wa Zuchu.
Alichofanya Mondi kuchanganya ladha ya zamani na sasa na kupata utamu wa leo jambo hilo kwa wanamuziki wa Dansi linashindikanaje?
Leo hii ukiisikiliza Waah ni kama imebeba makundi yote ya wazee na vijana; kila mtu anapata utamu wake na kuinjoi maisha, kifupi ni utamu kolea.
Hivi ndivyo Dunia ya leo inavyotaka; "akili zinazoendana na majira lazima zitumike ili kupata matokeo mazuri."
Tofauti na hapo, wanamuziki wa dansi mtaendelea kulia njaa huku wenye akili zao kama akina Mondi wanaongelea kwenye bwawa lenu la Dansi na kujichotea pesa kama zote.
Dunia ya leo haihitaji mtu wa kulalamika, bali wa matendo. Mondi ameonesha matendo, ametoboa na ndivyo ambavyo amekuwa akifanya mwanamuziki Christian Bella wa Malaika Band. Akiona gia ya Dansi imegoma kidogo anageuza upande anapiga miksa hatari ya Dansi na Bongo Fleva, anatoboa na kuendelea kula bata.
Sikiliza tungo za Bella kama Ninakuhitaji, Only You, Nashindwa na Msaliti, utagundua ninachomaanisha.
Ni matarajio yangu Wimbo wa Waah utageuza upepo wa Dansi kutoka ule wa kuimba kizamani na kuwa wa kisasa.
Namtarajia rafiki yangu, Ali Choki ataachana na biti za enzi za enzi za Kisa cha Mpemba na kuingiza za kileo ili kuteka mioyo ya vijana na bila shaka wa kale nao watamfurahia Choki aliyewaburudisha enzi za ujana wao.
Namshauri mdogo wangu, Chalz Baba ajifunze kuendana na matakwa ya vijana wenzake.
Huu ni wakati wa kuziona bendi zetu zikitunga nyimbo fupi, siyo zile za dakika 12, zenye midundo ya kisasa zilizochanganywa na ala za zamani.
Ni muda wa kuboresha muziki bila kuacha asili kama alivyofanya Mondi na Le Grand Mopao.
0714 895 555.
IMEANDALIWA NA RICHARD MANYOTA