Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Aboubakar Kunenge amewahakikishia wakazi wa Kifuru na Chanika kuanza kupata huduma Bora za Maji safi ifikapo Disemba 31 ikiwa ni utekelezaji wa agizo na ahadi aliyotoa Rais Dkt. John Magufuli kwa Wananchi wakati wa mkutano wa kampeni Jijini humo.
RC Kunenge leo akiambatana na Kamati ya usalama ya Mkoa na watendaji wa DAWASA wamefanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo ambapo wameshuhudia Mradi wa Ujenzi wa tank la maji lenye uwezo wa kupokea lita milioni mbili kwa siku likiwa limekamilika kwa 100% ambapo litakuwa likipokea maji kutoka Wilaya ya Kisarawe na kutawanya kwa wananchi wa Kifuru, Chanika, Banana, Gongolamboto na Pugu.
Aidha RC Kunenge ameonyesha kuridhishwa na hatua ya Ujenzi ulipofikia ambapo Hadi Sasa DAWASA wamefanikiwa kulaza mabomba kutoka Kisarawe Hadi Pugu urefu wa Km 4.5 hivyo kazi iliyobakia ni kulaza mabomba kutoka tank lilipo na kuyatawanya kwa Wananchi.
Hata hivyo RC Kunenge amewapongeza DAWASA kwa juhudi wanazofanya na kuwaagiza kuongeza kasi ili Mradi huo ukamilike kwa wakati sahihi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kwa Sasa Vijana wanaendelea na kazi ya kuhakikisha ifikapo Disemba 31 maagizo yote ya Rais Dkt. John Magufuli yanakuwa yametekelezwa kwa Vitendo.
Aidha Mhandisi Luhemeja amesema uwepo wa Mradi huo pia umekuwa mkombozi kwa wananchi kupitia fursa kubwa ya ajira iliyotolewa kwa vijana wazawa.