Maafisa wa Uturuki wamelikosoa vikali jarida la Charlie Hebdo la Ufaransa kwa kuchapisha kibonzo kinachomdunisha rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
Wamelituhumu jarida hilo kwa kuchochea chuki.Kibonzo hicho kimezidisha mzozo kati ya Uturuki na Ufaransa ambao ulianza baada ya msimamo wa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron dhidi ya Uislamu kuhusu uhuru wa mawazo na kujieleza, baada ya mwalimu aliyewaonyesha wanafunzi vibonzo vya Mtume Mohammed kuchinjwa.
Vibonzo vya Mtume Mohammed vimewaghadhabisha wengi katika ulimwengu wa Kiislamu. Lakini Erdogan ndiye alikuwa mstari wa mbele dhidi ya Ufaransa na kutilia mashaka hali ya afya ya akili ya Rais Macron. Matamshi ya Macron pia yalichochea maandamano na wito kwa Waislamu kuzisusia bidhaa za Ufaransa.