Watu wengi wameandamana katika nchi nyingi za Kiislamu baada ya sala ya Ijumaa leo, kuonyesha hasira zao dhidi ya namna Ufaransa inavyoishugulikia michoro ya vibonzo vya Mtume Mohammed.
Miongoni mwa miji iliyoshuhudia maandamano makubwa ni Gaza katika mamlaka ya Wapalestina, mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, na mji mkuu wa Pakistan, Islamabad.
Katika Ukanda wa Gaza, mmoja wa viongozi wa chama cha Hamas Fathi Hammad amewataka waandamanaji kuungana kukabiliana na alichokiita ''mashambulizi ya kihalifu'' yanayomlenga mtume.
Maandamano mengine yamefanyika baada ya sala katika msikiti maarufu wa al-Aqsa kwenye mji mkongwe wa Jerusalem mashariki, huku waandamanaji wakipaza sauti zao na kusema ''Tunaitikia wito wako mtume.''
Maandamano yamefanyika pia katika miji mikubwa ya nchini Pakistan, ambako waandamanaji walizochoma moto picha za rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na kutaka balozi wao nchini Ufaransa aitwe nyumbani.