Tuesday, July 7, 2020

Huyu Ndiye Sallam Mendez Aliyekataa Mkono wa Harmo!


KWENYE ulimwengu wa soka, kuna mtu hatari aitwaye Jorge Mendez. Ni mzaliwa wa pale jijini Lisbon, Ureno. Huyu ni wakala wa wanasoka wakubwa duniani kama Jose Mourinho, Felipe Scolari, Carlos, Anderson, Fabio Coentrao, Pepe, Angel Di Maria, Cristiano Ronaldo, Radamel Falcao, Ricardo Carvalho, Nani, Ricardo Quaresma, Burak Yilmaz, Joao Moutinho, James Rodriguez, David de Gea, Victor Valdes, Pedro na wengine wengi.

Huyu Jorge Mendez anatajwa kuwa mtu anayejua figisufigisu na fitina mno kwenye madili ya uhamisho wa wachezaji wakubwa kutoka timu moja kubwa kwenda nyingine duniani.

Jorge Mendez anatajwa kama mtu hatari zaidi kwenye eneo hilo na amekuwa tajiri mkubwa kutokana na madili hayo.

Tabia hiyo ya Jorge Mendez, imemfanya mtu aitwaye Sallam Sharrif 'SK' hapa Bongo, naye kupachikwa jina la Mendez kutokana na kuwa na tabia kama hizo.

Huyu Sallam ni mmoja wa mameneja wa mwanamuziki Nasibu Abdul 'Diamond Platnumz'. Ukubwa wa Diamond au Mondi kwenye muziki wa Afrika unafahamika. Mameneja wengine wa Mondi ni Hamis Taletale 'Babu Tale' na Said Fela 'Mkubwa na Wanawe'. Tofauti na wengine, huyu Sallam anaongoza kwa kuchukiwa mitandaoni.

NI NANI HASA HUYU SALLAM?

Kutoka lile tukio la kudaiwa kusababisha mwanamuziki Ali Saleh Kiba 'King Kiba' kuzimiwa maiki jukwaani pale Mombasa nchini Kenya; Oktoba 8, 2016 mbele ya mwanamuziki mkubwa duniani, Chris Brown hadi kukataa mkono wa mwanamuziki Rajab Abdul 'Harmonize' pale Morogoro wiki iliyopita, kila mtu anajiuliza huyu jamaa ni nani hasa?

OVER ZE WEEKEND imechimba na hapa inakuletea safari nzima ya Sallam kwenye Bongo Fleva, figisufigisu anazohusishwa nazo na tabia zake zinazodaiwa zitaupeleka muziki huu kaburini;

Sallam anatajwa kuwa mmoja wa watu muhimu mno kwenye menejimenti ya Mondi. Sifa yake kubwa ni mtu mzuri wa kutengeneza connections nyingi zilizompaisha Mondi kimataifa.

Mashabiki wengi wa Mondi na wadau wa Bongo Fleva hawamfahamu kiundani. Lakini huyu jamaa ni mzaliwa wa jijini Dar na siyo Morogoro kama baadhi ya watu wanavyodhani.

SALLAM NA MOROGORO

Kule Morogoro, Sallam alikwenda kusoma tu, kabla ya kujiingiza kwenye Bongo Fleva enzi hizo wakati muziki huu unaibuka.

Kama ulikuwa hujui, Sallam alianza kujiingiza kwenye muziki akiwa Shule ya Sekondari ya Forest pale Morogoro akiwa anarap.

Alikuwa na kundi lake la kurap lililoitwa Watukutu akiwa na Swedi na Puzzo. Wakati huo, Sallam alifahamika kwa jina la kisanii la OG. Watukutu lilileta ushindani kati ya wasanii wa Dar na Morogoro. Wale wa Dar walikuwa ni akina Sugu, Hard Blastaz na Dilpomatz.

UANDAAJI WA SHOO

Baadaye, kundi hilo lilisambaratika ambapo Sallam aliamua kujikita kwenye uandaaji wa shoo. Baada ya kuandaa shoo za ndani na kupata uzoefu, alianza uwakala wa kuleta wasanii wa nje ya nchi kuja kufanya shoo na kolabo na wasanii wa Bongo.

Hapa ndipo alipofanikiwa kuwaleta wasanii kama Prezzo na Huddah (Kenya) na J Martins (Nigeria). Baada ya shoo, J Martins akafanya kolabo na AY na MwanaFA kwenye ile Ngoma ya Bila Kukunja Goti na Ommy Dimpoz kwenye Ngoma ya Tupogo.

KOLABO YA MONDI NA DAVIDO

Baadaye alimshusha Bongo msanii Davido kutoka Nigeria, ndipo akafanikisha ile kolabo ya Mondi na jamaa huyo ya Number One Remix na kuanzia hapo akaanza na Mondi.

FIGISUFIGISU

Unaikumbuka ile Shoo ya Tigo iliyofanyika Viwanja vya Leaders jijini Dar, miaka mitano iliyopita? Shoo ile iliwajumuisha Mondi na Kiba jukwaani na haijatokea tena hadi leo. Shoo ile iliweka rekodi nyingi kuanzia vurugu nje ya uwanja na hata ndani kutokana na kuwepo kwa makundi mawili makubwa. Team Kiba ilikuwa na kazi moja tu; kumzomea Mondi. Team Mondi na yenyewe ilikwenda mbali zaidi kwa kuzomea na kumrushia Kiba chupa za maji?

Baada ya shoo hii, ndipo Sallam alipoanza kuonesha figisufigisu dhidi ya mahasimu wa Mondi. Baada ya shoo ile ambayo Kiba alikimbiza, kesho yake, Sallam aliweka kijiji pale Twitter akimtukana Kiba kuwa ni mchawi na muoga. Alikwenda mbali zaidi na kutoa madai kuwa Kiba na timu yake waliruka ukuta kuingia Viwanja vya Leaders.

Pia alidai Kiba hakumsalimia msanii yeyote. Hapo ndipo utashikwa na mshangao kwamba mambo ya Kiba kuruka ukuta na kutomsalimia msanii yeyote kama ni kweli au si kweli, yeye Sallam ilimhusu nini? Mbona wasanii wengine au mameneja wao hawakuzungumza, kwa nini yeye imuume kiasi kile na kukimbilia Twitter kumchafua Kiba?

SHOW YA CHRISS BROWN

Tukio lingine ni ile shoo ya Chriss Brown pale Mombasa ambapo Sallam alinaswa nyuma ya jukwaa na kudaiwa kufanya figisufigisu kumharibia Kiba kwa kuwa msanii wake Mondi hakupata chansi hiyo ya kufanya shoo mbele ya Chriss Brown.

Kiba alitakiwa afanye shoo ya live. Timu yake ilipaswa kufunga vifaa vya shoo ya live ambapo zoezi hilo lingechukua nusu saa halafu ndipo Kiba apande kufanya shoo. Hapa tatizo halikuwa kwa Kiba, bali kwa waandaaji wa shoo na fundi mitambo ambao walichelewa kufunga mitambo yao, hivyo Kiba alipopanda akaimba nyimbo mbili kisha akazimiwa maiki.

Baada ya kushuka jukwaani, Kiba alisema; "Nilimuona bosi wa Diamond, Sallam akiwa back stage (nyuma ya jukwaa) wakati ninashuka stejini. Kwa maana hiyo, Sallam alikuwa back stage wakati mimi ninapafomu, lakini ninajiuliza mwenyewe, Sallam alifuata nini back stage wakati mimi ninapafomu na ikiwa inafahamika mimi na wao hatuna maelewano mazuri? Unadhani watu watachukuliaje yeye kukaa back stage wakati mimi ninapafomu? Yeye ni nani mpaka akae back stage kwangu? Kama angetaka kuangalia shoo, si angekaa VIP aangalie shoo? Kwa nini aje back stage?"

Baadaye kuliibuka madai kwamba, Sallam alikula mchongo na meneja wa msanii Wizkid wa Nigeria aitwaye Mr Sande ambaye pia ni meneja wa Mondi kwa Afrika Magharibi, wakashirikiana kumhujumu Kiba.

TUKIO LA COKE STUDIO

Kuna kipindi Kiba alikwenda Coke Studio pale Nairobi ambapo aliungana na mwanamuziki wa Marekani, Neyo ambaye alikuwa yupo tayari kufanya naye kolabo.

Kuna madai kwamba, usiku wa tukio hilo, baada ya Sallam kuinyaka ishu hiyo, hakulala, alifunga safari usiku huohuo kwenda Nairobi. Alipofika kule alidaiwa kumtia maneno Neyo na kuvuruga kabisa mipango yote ya Kiba na Neyo. Unajua nini kilifuata? Neyo alifanya kolabo ya Ngoma ya Marry You akiwa na Mondi. Huyo ndiye Sallam Mendez!

KUKATAA MKONO WA HARMO

Tupo msibani Morogoro kumpumzisha kwenye nyumba ya milele mke wa Babu Tale, Shamsa Kombo 'Shammy' aliyefariki dunia wiki iliyopita.

Inafahamika kwamba mwishoni mwa mwaka jana, mwanamuziki Rajab Abdul 'Harmo' alijitoa kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya Mondi. Kumbe kuondoka kwa Harmo kulimuacha Sallam na kinyongo au gubu, jambo ambalo ni baya mno hasa likifanywa na mtoto wa kiume!

Harmo anafika msibani na kusalimiana na watu wa kila aina, lakini anapofika kwa Sallam, jamaa anakataa kumpa mkono. Harmo anabaki amegandisha mkono akiwa amemnyooshea Sallam anayejifanya yupo bize na simu kisha kutaka kuupiga mkono huo ili Harmo aondoke mbele yake. Watu wanapatwa na mshangao!

Watu wanamshangaa Sallam kuonesha bifu msibani. Harmo anajisikia vibaya, lakini anaamua kuchukulia poa kwa sababu mbona mameneja wengine wa Wasafi walisalimiana vizuri tu? Kwa nini Sallam anaonesha tabia za kitoto msibani? Kwa nini Sallam anaonesha tabia za Kiswahili msibani? Kwa nini Sallam anaonesha chuki msibani? Jibu ni moja tu;

Huyu ndiye Sallam Mendez anayepaswa kujitafakari, yeye anajiona shujaa wa kuifikisha Bongo Fleva kimataifa, lakini si ajabu anaichimbia kaburi kwa tabia zake!

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...