Tuesday, July 14, 2020

EPL: Obafemi ainyima Manchester United fursa ya kuingia 4-bora




MSHAMBULIAJI Michael Obafemi, 20, alitokea benchi katika kipindi cha pili na kufungia Southampton bao la kusawazisha kunako dakika ya 96 katika sare ya 2-2 dhidi ya Manchester United.
Matokeo hayo yaliyosajiliwa na The Saints uwanjani Old Trafford yaliwanyima Man-United fursa ya kupaa hadi nafasi ya tatu kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 61 na hivyo kuweka hai matumaini ya kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora.
Man-United kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano kwa pointi 59 sawa na Leicester City wanaoorodheshwa mbele yao kutokana na wingi wa mabao.
Ilivyo, matumaini ya Man-United ya kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao, yanategemezwa kwa matokeo yatakayosajiliwa na Chelsea na Leicester katika mechi zao tatu za mwisho. Kujikwaa kwa Chelsea na kuteleza kwa Leicester katika mchuano wowote kati ya hiyo mitatu kutawapa Man-United uhakika wa kuwa miongoni mwa washiriki wa kivumbi cha UEFA mnamo 2020-21.
Licha ya kuchezea ugenini, Southampton walianza mechi kwa matao ya juu na wakajiweka kifua mbele kupitia kwa Stuart Armstrong aliyechuma nafuu kutokana na masihara ya Paul Pogba na kutikisa nyavu katika dakika ya 12.
Bao hilo la The Saints liliamsha hasira za Man-United waliosawazisha kupitia kwa Marcus Rashford kunako dakika ya 20 kabla ya Anthony Martial kufunga la pili dakika tatu baadaye.
Ilikuwa hadi mwishoni mwa kipindi cha pili, sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi ambapo Obafemi alijaza kimiani mpira wa ikabu uliochanjwa na Jan Bednarek na kuhakikisha kwamba wanaoondoka ugenini na alama moja kikapuni.
Ilitarajiwa kwamba kichapo cha 3-0 ambacho Chelsea walipokezwa na Sheffield United uwanjani Bramall Lane mnamo Julai 11 na kile cha 4-1 ambacho Bournemouth waliwapa Leicester City siku hiyo hiyo ugani Vitality, kingekuwa kiini cha hamasa ya Man-United hiyo iliyowakutanisha na The Saints.
Hata hivyo, kikubwa zaidi ambacho bado kinawaaminisha Man-United kuwa watakamilisha kampeni za EPL msimu huu miongoni mwa vikosi vinne vya kwanza, ni uzito wa vibarua vilivyopo mbele ya Chelsea na Leicester.
Baada ya kuvaana na Norwich City leo Julai 14 uwanjani Stamford Bridge, Chelsea watakuwa na mtihani mgumu dhidi ya Liverpool na Wolves katika michuano yao miwili ya mwisho. Mechi hizi za mwisho zitapigwa baada ya Chelsea kupimana ubabe na Man-United katika nusu-fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley mnamo Julai 19.
Leicester nao wana kibarua kikali cha kuwazidi maarifa Sheffield United uwanjani King Power kabla ya kuwaendea Tottenham kisha kupimana ubabe na Man-United katika mechi yao ya mwisho wa msimu huu ugani King Power.
Kwa upande wao, Man-United wanatarajiwa kuwa na mteremko mkubwa dhidi ya Crystal Palace na West Ham United kabla ya kufunga msimu dhidi ya Leicester waliotawazwa mabingwa wa EPL mnamo 2015-16.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...