Friday, May 29, 2020

Zitto Kabwe kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kutoa matamshi ya uchochezi



Kiongozi wa chama cha upinzani ACT-Wazalendo nchini Tanzania ametiwa hatiani na mahakama jijini Dar es Salaam na kuhukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja kwa sharti la kutotoa kauli za kichochezi. 

Chama chake cha ACT tayari kimetoa taarifa ya kuwa bwana Kabwe anapanga kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo. 

Mahakama hiyo imemtia hatiani Zitto kwa makosa yote matatu ya uchocheji yaliyokuwa yanamkabili. 

Hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi imekuja baada ya kipindi cha zaidi ya mwaka mzima wa kesi kuunguruma, kwa mara ya kwanza bwana Zitto kufikishwa mahakamani kusikiliza kesi zake ilikuwa Novemba 2, mwaka 2018.

Zitto anadaiwa kutenda makosa hayo ya uchochezi Oktoba 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari. 

Chama cha ACT kupitia makamu mwenyekiti wake Dorothy Semu kimetoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa hukumu dhidi ya kiongozi wao haikubaliki na wataipinga mahakamani. 

"Hukumu hii ni sawa na kumzuia Zitto kusema chochote cha kuikosoa serikali na rais katika mwaka wa uchaguzi," inaeleza sehemu ya taarifa ya Bi Semu. 

"Hukumu hii haiwezi kukubalika. Inaweza kuwa mfano wa kuminya uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza Tanzania."

Bi Semu ameituhumu serikali ya chama tawala nchini Tanzania CCM kwa kile alichokiita "kutumia mashtaka ya uchochezi kuwanyamazisha wale wanaongea ukweli dhidi ya serikali.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...