KWA kipindi cha kati, wasanii wengi na watu maarufu walikuwa na tabia ya kupenda kusafiri nje ya nchi aidha kwa kufanya biashara au kula bata. Lakini kwa sasa ghafla upepo umebadilika, badala ya kwenda na kurudi, wengi wao wameshahamisha na kambi mazima huko.
Wapo wasanii ambao awali walikuwa huko lakini walikuwa wakija Bongo na kufanya kazi zao kama kawaida, ambapo wengi waliamini kuwa ukiwa nje ya nchi, basi unaenda kujifunza mambo mengi yahusuyo sanaa na hatimaye kukua, lakini kwa sasa wameibuka wasanii wengi ambao wanaishi nje ya nchi na hatimaye kuweza kudorora kwenye sanaa zao.
Makala haya yanakudadavulia orodha ya mastaa ambao kabla ya kutoka Bongo, walikuwa wakifanya poa kunako kwenye anga la muziki au filamu Bongo, lakini baada ya kuondoka tu, mambo yakabadilika na kuwa kimya:
HUSSEIN MACHOZI
Ni msanii wa muziki wa Bongo Fleva, ambaye alitamba sana katika kipindi cha miaka ya 2000. Ngoma ya kwa Ajili Yako na Kafia Ghetto, ndizo zilizomtambulisha na hatimaye raia kuweza kumkubali hadi kujulikana.
Baada ya hapo akaachia ngoma kama; Utaipenda akimshirikisha Joh Makini, Maji Yakimwagika, Hello aliyomshirikisha Maunda Zoro na nyinginezo, ambazo alizotoa akiwa hapahapa nyumbani.
Baada ya hapo, akaanzisha maisha mengine nchini Italy huku akiendeleza saana yake ya muziki, ambapo mnamo 2015 aliweza kuachia kibao cha Msinitimue. Pamoja na kwenda nje ya nchi, lakini bado kazi zake anazozitoa hazina nguvu kama zilivyo kazi zake zilizopita.
RAY C
Ni mkongwe ambaye alitamba kwa albamu ya Mapenzi Yangu mwaka 2003, ikiwa na mjumuiko wa ngoma kali kama Sikuhitaji, Na Wewe Milele, Mapenzi Yangu, Ulinikataa, Sogea Sogea, Uko Wapi, Touch Me nakadhalika.
Sambamba na albamu hiyo, aliweza kutwaa tuzo mbili nchini na moja ya Afrika Mashariki. Kabla ya kutopea kwenye matumizi ya madawa ya kulevya, alikuwa akifanya freshi. Lakini baada ya kutoka kwenye matumizi hayo, 2018 aliweza kuachia ngoma ya Roga Roga, ambapo alikuwa akiishi hapa hapa nchini.
Baada ya kwenda nje ya nchi, ghafla akaanza kupotea kwenye sanaa yake. Kwani tangu atoe ngoma yake ya mwisho mwaka 2018, hadi leo hajatoa ngoma nyingine, na wala ngoma yake hiyo haikufanya vizuri kama ngoma zake nyingine zilizopita.
DIANA KIMARI
Ni msanii kutoka kiwanda cha filamu Bongo, awali watu waliweza kumfananisha na muigizaji mwenzake Elizabeth Michael 'Lulu' kwa kuwa walikuwa wakielekeana kwa umbo na hata rika lao. Aliweza kufanya muvi nyingi na zenye kiwango cha hali ya juu akishirikiana na wasanii wakubwa wenye majina kama marehemu Steven Kanumba, Vincent Kigosi 'Ray', Lulu, na wengineo.
Kabla ya kuzamia Marekani, Diana alijulikana sana, lakini baada ya kwenda huko amekuwa kimya kwenye sanaa hiyo, badala yake amekuwa akiposti picha tu mitandaoni akila bata huku kazi zikiwa hazionekani.
VANESSA MDEE
Umbile, sauti pamoja na jitihada zake, vimeweza kumfanya Vanessa Mdee kuwa miongoni mwa wasanii wa kike wanaopendwa na watu wengi nchini. Kwani vimeweza kumfanya kuimba vizuri pamoja na kupafomu vilivyo jukwaani hadi kukonga nyoyo za mashabiki zake.
Kabla ya kuanzisha mahusiano mapya na Mpenzi wake Rotimi, alikuwa hapa nchini akifanya kazi zilizokubalika na kutikisa vilivyo kama Hamjui, Kisela, Niroge, Siri, Bounce, Game na nyinginezo. Lakini baada ya kuzama kwa mpenzi wake huyo Marekani, hakuna kazi yoyote aliyoitoa, badala yake amekuwa akiposti picha akila bata.
AY
Ni mkongwe kwenye tasnia ya muziki wa Bongo Fleva, ambaye aliingia kwenye fani hiyo mnamo miaka ya 2000. Tangu aingie kwenye gemu hilo hadi sasa, hajawahi kuchuja. Kwani nyimbo zake ni nzuri na zinakubalika mno na mashabiki wake.
Ukilinganisha nyimbo alizozitoa nyumbani na akiwa nje kama Zigo Remix akishirikiana na Diamond, Usijaribu na nyinginezo, zina watazamaji wengi, lakini wimbo alioutoa akiwa nje ya nchi wa Dan'Hela, bado haujafanya vizuri, kwa kuwa una watazamaji 28, 3724 ikiwa na miezi miwili tangu itoke. Hivyo, nje kumemfifisha msanii huyo.
HITIMISHO
Mbali na wasanii hao kufanya vibaya, pia kuna baadhi yao ambao wameweka maskani huko nje ya nchi na kufanya vizuri ambapo ROMA ni mmoja wapo.
Mchanaji huyu anafanya freshi kwenye anga la Hip Hop kwani kabla ya kuondoka nchini, aliweza kuachia ngoma kama Viva, Zimbabwe na nyingine aliweza kushirikiana na rafiki yake Stamina kwenye vibao kama; Parapanda, Kaolewa, Hivi ama Vile, Kibamia na nyinginezo.
Baada ya kutua nchini humo mwaka jana, mapema Januari 3, mwaka huu aliweza kuachia kibao cha Mkombozi kikiwa na jumla ya watazamaji 1,300,853 kwenye mtandao wa YouTube.
Kutokana na data hiyo, sanaa yake ameikuza kwa kupanua mashabiki kwani ngoma yake ya Zimbabwe aliyoitoa 2017 ina jumla ya watazamaji 2,648,535. Hivyo, nje kumemuimarisha. Ni vyema wasanii wengine waliopo nje kufuata njia alizopita msanii huyu.