Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Suleiman Masoud Suleiman maarufu Suleiman Nchambi (CCM) kwa tuhuma za kupatikana na silaha 10, risasi 536 na nyama zinazodhaniwa kuwa ni za wanyawapori kinyume cha sheria.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumatano Mei 6,2020, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea Mei 3,2020 majira ya saa sita kasoro usiku katika mtaa wa Lubaga kata ya Lubaga Manispaa ya Shinyanga.
"Mei 3,2020 majira ya sita kasoro usiku Kikosi kazi cha askari wa upelelezi kikiongozwa na Kaimu Mkuu wa upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoa wa Shinyanga SP Davis Msangi kwa kushirikiana na Afisa wa Wanyamapori mkoa wa Shinyanga Perfect Mbwambo walifanya upekuzi kwenye makazi ya Mbunge wa Jimbo la Kishapu baada ya kupata taarifa za kiintelejensia kuwa Mheshimiwa huyo alikuwa akifanya uwindaji haramu kwenye eneo la Negezi wilayani Kishapu akiwa na gari yenye namba za ujasili T760 DSD Nissan Hard Body",ameeleza Kamanda Magiligimba.
"Katika upekuzi huo walifanikiwa kukamata nyama iliyodhaniwa kuwa ni wanyamapori yenye uzito wa kilogramu 35 zikiwa zimehifadhiwa kwenye jokofu lililokuwa jikoni,jingine sehemu ya mazoezi na nyama nyingine ilikutwa kwenye gari hilo likiwa limeegeshwa nyumbani kwake ndani ya uzio wa nyumba hiyo",amesema Kamanda Magiligimba.
"Katika gari hilo kulikutwa silaha moja aina ya shortgunWakati askari hao wakiendelea na upekuzi ndani ya chumba chake cha kulala zilipatikana silaha zingine za aina mbalimbali na kufanya jumla ya silaha zilizokamatwa kuwa 16 ambazo ni Airgun 3, Shortgun 3,Rifle 8, Pistol 1 na Mark IV 1 pamoja na risasi 536 zikiwa kwenye kabati la nguo",anaeleza Kamanda.
"Baada ya uchunguzi wa awali iligundulika kuwa silaha 10 ambazo ni Airgun 2, Rifle 5, Shortgun 2 na Mark IV 1 kati ya 16 anazimiliki isivyo halali",ameeleza Kamanda Magiligimba.
Kamanda Magiligimba amesema nyama hizo zimepelekwa maabara ya mkemia mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi na gari husika limekamatwa.
"Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika. Natoa onyo kali kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kumiliki silaha isivyo kihalali hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake",amesema Kamanda Magiligimba.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa Mbunge wa Jimbo la Kishapu Suleiman Masoud Suleiman
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba akionesha kwa waandishi wa habari silaha alizokamatwa nazo mbunge wa Jimbo la Kishapu Suleiman Masoud Suleiman
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba akionesha kwa waandishi wa habari silaha alizokamatwa nazo mbunge wa Jimbo la Kishapu Suleiman Masoud Suleiman
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba akionesha kwa waandishi wa habari risasi alizokamatwa nazo mbunge wa Jimbo la Kishapu Suleiman Masoud Suleiman