Friday, March 27, 2020

Yanga, GSM Mambo Safi, Niyonzima Afunguka


BAADA ya kuenea taarifa za kujitoa kwa wadhamini wa Klabu ya Yanga, Kampuni ya GSM, kiungo mchezeshaji wa timu hiyo, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ameibuka na kusema kuwa ni wakati sasa kwa uongozi kuwaachia timu wadhamini hao ambao wamefanikisha mambo mengi ndani ya muda mfupi.

Mapema jana zilienea taarifa za GSM kujitoa katika sehemu ya udhamini wa timu hiyo ikiwemo kuwezesha usajili wa wachezaji baada ya kuwepo malalamiko kwa baadhi ya viongozi kutoshirikishwa katika usajili wa wachezaji akiwemo Mghana, Bernard Morrison.

Hata hivyo, Spoti Xtra limepata taarifa za uhakika kwamba, jana jioni viongozi wa Yanga walikutana na watu wa GSM kujadili ishu hiyo na mambo yakaenda sawa. Yanga kupitia kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati maalumu ya kukusanya michango ya kusaidia timu hiyo, ndiye aliyekutana na mmiliki wa GSM, Gharib Said Mohamed.

"Ishu ya GSM na Yanga hivi sasa imekaa sawa, zile tetesi za kwamba wadhamini wetu hao wanataka kujiweka pembeni imeisha, kwani jana walikutana viongozi wa Yanga na wa GSM, mazungumzo yakaenda sawa," kilisema chanzo.

Niyonzima ambaye jana Jumatano alitembelea Ofisi za Global Publishers zinazochapisha Gazeti la Spoti Xtra, alifanya mahojiano kusema: "Kwa upande wangu naweza nikasema GSM wapewe kipaumbele kwani wanatuwezesha vitu vingi kwenye timu, ukizingatia kwa kila mechi tunazoshinda wanatupatia Sh Mil 10, kama hamasa wakati kwenye timu tunapewa shilingi laki moja.

"Natamani GSM waachiwe Yanga kutokana na sapoti yao kubwa wanayoitoa kwenye timu kwani kwa kiasi kikubwa wametufanyia mambo mengi ambayo hata wenyewe mnayaona na mengine hatuwezi kuyazungumzia hapa."

Aidha kiungo huyo aliongeza kuwa, endapo uongozi wa timu hiyo utaruhusu mdhamini huyo kujitoa kwa kiasi kikubwa timu hiyo itayumba kiuchumi kutokana na wadhamini hao kuwezesha mambo mengi kama kulipa posho, mishahara na kusimamia usajili wa wachezaji.

Katika hatua nyingine, Niyonzima aliwataka viongozi wa timu hiyo kupambana kuhakikisha wanambakisha kiungo, Papy Tshishimbi kwa kumuongezea mkataba na wasimuachie aende Simba. "Wanapoondoka wachezaji wakongwe na wazoefu kunaidhoofisha timu, hivyo uongozi utalazimika kutengeneza upya timu kitu ambacho ni kibaya, kwangu Tshishimbi ni kati ya wachezaji muhimu wanaotakiwa katika timu," alisema Niyonzima.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...