Friday, March 27, 2020

Bosi wa TAKUKURU Kinondoni, wenzake wanne wakalia kuti kavu

 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania imesema itawakamata watumishi wake watano akiwamo mkuu wa taasisi hiyo Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Teddy Mjangira ili kujibu tuhuma zinazowakabili.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Machi 26, 2020 kwa simu, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo amesema watumishi hao kwa pamoja wanatuhumiwa kumfanyia uchunguzi mtumishi wa umma ambaye hakuwa na kosa.

Amesema hatua hiyo ilimsababishia usumbufu usiokuwa wa lazima.
"Tutawakamata, tutawaweka ndani na tutafanya uchunguzi kujua hasa nini kilitokea. Lakini niseme tu kuwa utumishi wa umma unahitaji kuwa na maadili na nidhamu na tuna imani mkuu wetu (wa Kinondoni) amepotoka," amesema Mbungo

Mapema leo Alhamisi asubuhi, Rais wa Tanzania, John Magufuli wakati akipokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2018/19 na ya Takukuru ya mwaka 2018/19 Ikulu ya Chamwino, Dodoma aliipongeza taasisi hiyo ya ukaguzi huku akigusia watumishi hao wa Kinondoni bila kufafanua zaidi.

Kutokana na utendaji mzuri wa Takukuru, Rais Magufuli amemdhibitisha Brigedia Jenerali John Mbungo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.

Awali, Mbungo alikuwa akikaimu nafasi hiyo yangu Septemba 12, 2019 baada ya aliyekuwa mkurugenzi mkuu, Diwani Athuman kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...