Thursday, September 19, 2019

MAMBO Manne (4) Ya Kimafanikio Ya Kumfundisha Mtoto Wako Mapema...!!!


Msingi mkubwa wa mafanikio ya mtu yeyote kitabia unatokana na malezi bora aliyopata hasa akiwa mtoto kuanzia mwaka mmoja hadi miaka kumi na mbili. Katika kipindi cha mwaka 1 hadi 12 ndio kipindi muhimu sana cha malezi.

Tabia nyingi ambazo zinatengenezwa au kufundishwa katika kipindi hiki, huwa kuna uwezekano mkubwa wa kudumu maishani mwako kote. Hapa hii inatokea bila kujali tabia hiyo ni nzuri kwako au mbaya.

Kwa mfano, kama ulikuwa unaendekeza uvivu au kama ulikuwa mtu wa kuchapa kazi sana na kujiona huo ndio kama utamaduni katika kipindi cha mwaka 1 hadi 12, ni rahisi tu tabia hizo kuendelea hadi ukubwani.

Kwa mantiki hiyo ndiyo maana ni muhimu sana kumfundisha mtoto wako mambo ya kimafanikio yatakayomsaidia  kwa baadae kwenye maisha yake. Mambo hayo ni yepi? Karibu na twende pamoja tujifunze.   

1. Mfundishe, njia bora ya kufikiri.

Ikiwa hupendi sana maisha yako yalivyokuwa mwanzoni yaendelee kwa kizazi chako, sasa ni wakati wa kumfundisha mtoto wako namna bora ya kufikiri. Hapa ni lazima umfanye mtoto wako aweze kufikiri chanya.

Unaweza kumfanya moto wako afikiri chanya kwa kumpa vitabu vizuri chanya kama uwezo wa kusoma anao au kwa maneno maneno unayomwambia. Hiyo haitoshi pia unaweza ukamtafutia marafiki wazuri wenye mtazamo chanya.

Kama mtoto wako unamlea kwa mtazamo chanya, kufikiri kwa njia bora itakuwa kwake ni jambo ambalo halikwepeki. Anza leo kuweka mikakati yakumjengea mwanao njia bora ya kufikiri itakayomsaidia hata kumjengea mtazamo chanya pia.

2. Mfundishe, kujitegemee mapema.

Kati ya kitu kitakachofanya ujenge msingi imara kwa watoto wako kwa baadae ni kule kufanya wajitegemee mapema. Hapa inatakiwa umfundishe mtoto wako kufanya baadhi ya mambo mwenyewe.

Kwa mfano, anapokuwa mkubwa kidogo kama ni kufua mwache afue mwenyewe. Kama ni kusaidia kazi fulani acha aifanye. Njia hii inakuwa bora kwa kujua kwamba kuna vitu fulani anatakiwa awajibike.

Lakini kama utakuwa ni mtu wa kumlea mtoto wako kwa kutaka kila kitu  afanyiwe basi wewe ndiye utakuwa mtu wa kwanza kumharibu mtoto wako. Mfanye mtoto wako ajitegemee mapema, 
itamsaidia sana kwa baadae katika makuzi yake.

3. Mfundishe, ajifunze kuchukua hatua mapema.

Siku zote vitendo ni bora sana kuliko kusema. Kwa kuwa unajua umuhimu wa hili anza kumfundisha mtoto wako juu ya umuhimu wa kuchukua hatua mapema katika maisha yake hata kwa vitu vidogo ambavyo anavyofanya.

Kwa kumfundisha hivi unakuwa unajenga utamaduni imara ambao utamfanya mtoto wako hata atakapokuwa mkubwa atakuwa anajua na kutambua umuhimu wa kuchukua hatua mapema pia kwenye maisha yake.

Ili hili lifanikiwe, mfundishe kitu fulani halafu anza kufatilia utekelezaji. Unaweza ukamwacha hata maswali kama kazi ya nyumbani, halafu uone atamaliza baada ya muda gani? Utakuwa unafanya hivyo mara kwa mara ili kumfanya achukue hatua mapema zaidi.

4. Mfundishe ajue mambo yote huwa hayaendi kama yalivyopangwa.

Katika kumfundisha atambue kwamba mambo kuna wakati hayaendi kama yanavyopangwa, subiri kipindi ambapo anataka kitu fulani tena kwa hamu kubwa. Inapofika katika hicho kipindi kwa makusudi mnyime.

Najua kama ilivyo kwa watoto walio wengi tabia zao atalia. Mwache alie halafu tafuta siku ama muda akitulia, kama kile kitu kilikuwa cjha kununua, mnunulie na mpe somo mapema atambue kuna wakati mambo hayaendi moja kwa moja kama uliyopanga.

Fanya hivi kwa mtoto ambae ameshaanza kujitambua ikiwezekana kuanzia angalau darasa la tano. Rudia tena na tena zoezi hili, mpaka ifike mahali ajue kwamba mategemeo na uhalisia ni vitu viwili tofauti.

Yapo mambo mengi unayoweza kumfundisha mwanao ya kumweka juu kimafanikio kwa baadae. Unaweza kumfundisha mwanao pia jinsi ya kuishi na watu sahihi, uaminifu katika maisha, misingi bora ya kuishi maisha ya kiroho napengine hata faida ya kujiamini.

Fanyia kazi haya machache kwa leo na chukua hatua katika kuweza kufikia mafanikio yako makubwa.

Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
0713 04 80 35,
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...