Msanii wa Bongo Fleva, Dudu Baya ameipigia magoti familia ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji, Ruge Mutahaba akiomba radhi kwa maneno ya kashfa aliyoyatoa dhidi ya nguli huyo katika tasnia ya habari wakati wa msiba.
Dudu Baya ametumia mtandao wa Instagram kuomba familia ya marehemu, Serikali pamoja na Watanzania kwa ujumla kwa alichokifanya wakati wa msiba huo.
"Nachukua fursa hii kuomba radhi ikiwa ni mwezi wa Kwaresma, mwezi wa kuomba msamaha na mwezi wa kusamehe, naomba msamaha kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa na jamii nzima ya Watanzania, na Familia [ya Marehemu Ruge] na watu wote walioguswa kwa maneno ya dhihaka niliyoyatoa wakati msiba ulipotokea," amesema Dudu Baya.
"Naomba msamaha kwa moyo wa unyenyekevu nikiamini Mwenyezi Mungu amenisamehe, na watu wote niliowakosea naomba mnisamhe," ameongeza.
Dudu Baya alitoa maneno ya kashfa dhidi ya Marehemu Ruge, hali iliyosababisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kuliagiza jeshi la polisi pamoja na Basata kumchukulia hatua.
Msanii huyo alijisalimisha katika kituo cha polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam ambapo aliachiwa kwa dhamana baada ya siku kadhaa na amekuwa akiendelea kuripoti katika kituo hicho.
Basata walichukua hatua ya kusimamisha leseni yake ya sanaa, hali inayomfanya kutofanya kazi yoyote ya muziki.