Mwanafunzi wa kime wa darasa la saba Shule ya Msingi Ifukutwa Kata ya Mpanda Ndogo Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi Ephria Valeli Kijungu (15) amejinyonga kwa kujitundika juu ya mti wa mwembe kwa kutumia tisheti kwa kile kinachodaiwa kuchoshwa na manyanyaso ya wazazi wake walioshindwa kumhudumia mahitaji yake ya msingi.
Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa tatu subuhi jirani na nyumba waliyokuwa wakiishi na kaka yake ambaye ndiye alikuwa mlezi wa mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Damas Nyanda marehemu alikuwa akiishi na kaka na mke wa kaka yake ambapo kaka yake huyo aitwaye Edga Mpenda mara nyingi alikuwa akiishi kwenye mashamba yake na kumwacha mdogo wake nyumbani wakiwa wanaishi na shemeji yake.
Inaelezwa kuwa kabla ya kutokea kwa kifo chake alikuwa akiwaambia wanafunzi wenzake pamoja na majirani aliokuwa akiishi nao kuwa ipo siku atajinyonga tu kutokana na mateso anayoyapata hapo nyumbani kwao hivyo haoni sababu ya kuendelea kuishi ni bora afe ili apumzike.
Miongoni mwa mateso aliyokuwa akilalamikia ilikuwa ni kitendo cha yeye licha ya kuwa mwanafunzi huduma zote za msingi alizokuwa akizihitaji ilikuwa ni lazima ajihangaikie yeye mwenyewe kwa kufanya vibarua ndipo aweze kupata mahitaji yake na pia alikuwa akipata kichapo cha mara kwa mara kutoka kwa walezi wake hata pasipokuwa kufanya kosa lolote lile.
Kamanda Nyanda alisema kutokana na hali hiyo siku ya tukio marehemu alikuwa amelala ndani ya chumba chake na ndipo usiku huo alitoka chumbani kwake ambapo kaka yake na shemeji yake pasipo kujua kama ametoka ndani ya chumba aliyokuwa akiishi .
"Kulipokucha walezi hao waliamka na kuendelea na shughuli zao na hakukuwa na shaka yoyote ya juu ya mwanafunzi huyo mpaka ilipotimia majira ya saa tatu asubuhi mwili wa marehemu huyo ulipoonekana umening'inia juu ya mti wa mwembe jirani kidogo na nyumbani wanapoishi",alieleza Kamanda Nyanda.
Kufuatilia tukio hilo,Majirani walikusanyika kwenye eneo hilo na kisha kutoa taarifa kwa jeshi la Polisi Wilaya ya Tanganyika ambao walifika kwenye eneo hilo na kuukuta mwili wa marehemu ukiwa unang'inia juu ya mti wa mwembe.
Kamanda Nyanda alisema mwili wa marehemu ulichukuliwa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali teule ya Mkoa wa Katavi na baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa kidaktari mwili huo ulikabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi ambayo yalifanyika jana katika Kijiji cha Ifukutwa Kata ya Mpando Ndogo.
Mpaka sasa hakuna mtu au watu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo na polisi bado wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi juu ya kifo hicho.
Na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog
Na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog
Source