Upelelezi wa kesi inayomkabili Harbinder Sethi na James Rugemalira katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam bado haujakamilika.
Wakili wa Serikali, Iman Nitume ameeleza hayo jana Oktoba 11, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipotajwa, akidai upelelezi bado haujakamilika.
Baada ya wakili huyo wa Serikali kueleza hayo, wakili wa utetezi, Dora Mallaba ameomba upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo ili kesi ianze kusikilizwa.
Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja hizo ameiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 25, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
Washtakiwa hao wapo rumande tangu Juni mwaka jana kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana.