Thursday, October 11, 2018

Sumaye Aungana Mkono Kauli ya Katibu Mkuu wa CCM

Sumaye Aungana Mkono Kauli ya Katibu Mkuu wa CCM
Aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fredrick Sumaye ameunga mkono kauli ya Katibu Mkuu  wa CCM, Dkt. Bashiru Ally ya kuwa vitendo vya rushwa na kutowajibika vinasababisha watu kupuuzia uchaguzi na kuuona kama ni maigizo akidai kuwa kauli hiyo ni marudio.



Akizungumza na www.eatv.tv, Sumaye amesema kuwa ni kweli watu hawana imani na kura kwakuwa amezungumza Katibu Mkuu wa chama tawala hivyo amekubaliana na vyama vya upinzani maana jambo hilo wamekuwa wakilizungumzia mara kwa mara.

Sumaye amefunguka kuwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi sasa wananchi wamekuwa waoga kutokana na siasa za mihemko zilizoibuka hivi karibuni, tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

"Uchaguzi wa mwaka 2010 ambao Bashiru aliutumia kutolea mfano niliwahi kuzungumzia kipindi hicho mara tu baadaya kutangazwa kwa matokeo, kwakuwa CCM ilipata ushindi ambao ulikuwa finyu, kwakuwa asilimia ilikuwa 25 tu ya kura zilizoandikishwa", amesema Sumaye.

Sumaye ameongeza kuwa kauli ya Dkt. Bashiru isiishie hapo akishauri chama tawala pia kufuate yale aliyosema ili kurudisha imani kwa wapiga kura.

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally aliwahi kuzungumza kuwa vitendo vya rushwa na kutowajibika vimesababisha wananchi kupuuza uchaguzi na kuuona kama maigizo hivyo kupelekea idadi ya kura za chama chake kupungua kutokana na wapiga kura kutokuwa na imani na uchaguzi.

Dkt. Bashiru alitoa kauli hiyo Oktoba 4, 2018 mjini Morogoro katika Kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) alipokuwa akizungumzia kuhusu umuhimu wa wananchi kuiwajibisha serikali.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...