Saturday, October 20, 2018

SABABU ZA MO DEWJI KUTEKWA ZAANIKWA...MWENYEWE AFUNGUKA ILIVYOKUWA



Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Tanzania, Simon Sirro amesema waliomteka mfanyabiashara Mohammed Dewji 'Mo Dewji' walitaka kupewa fedha licha ya kutotaja kiwango wanachohitaji.

Sirro ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Oktoba 20, 2018 katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam ambako watekaji hao walimtupa bilionea huyo, kuendelea kuwasisitiza wananchi kutoa taarifa ili watekaji hao wakamatwe.

"Hii gari imetelekezwa na Mo Dewji ameachiwa lakini mwenyewe amesema wazi kuwa waliomteka waliomba fedha ila hawakusema ni kiasi gani," amesema Sirro.

''Mo ameniambia tangu alipotekwa alikuwa amefungwa mikono, miguu na kufunikwa macho, lakini pia walimsimamia sana kwenye suala la kula lakini sababu kubwa watekaji walikuwa wanataka fedha ila walikuwa na hofu ya kumpigia baba yake wakiamini jeshi la polisi litawafikia'', amesema Mambosasa.

Mambo sasa ameongeza kuwa baada ya taarifa za jana kutoka kwa IGP Sirro kubaini gari lililotumika kumteka, zimesaidia kumpata mfanyabiashara huyo kwani wahusika waligundua wamekaribia kunaswa.

Kamanda Mambosasa pia amethibitisha kuwa gari lenye namba za usajili T 314 AXX, ambalo walilibaini kutumika kumteka Mo, likiwa na namba za nchi jirani AGX 404 MC, ndio hilo limetumika kumtelekeza katika eneo la Gymkhana jijini Dar es salaam.

Amemaliza kwa kusema baada ya kutupwa pale Gymkhana, walinzi wa eneo hilo walimuona na kumtambua kama ni Mo, ndipo wakamfungua kamba alizokuwa amefungwa kisha akawatajia namba za simu za baba yake na walipompigia mzee Dewji akafika na familia kumchukua.

"Walitelekeza gari saa saba usiku (leo) na Mo aliwasiliana na baba yake ambaye alikuja kumchukua na tulivyokagua gari tulikuta lina silaha nne, bastola tatu, bunduki ya kivita aina ya AK 47 na risasi 19," amesema Sirro.

Amesisitiza, "Hii ni AK 47 ni salaha ya kivita na kuna uwezekano wametoka nayo kwao ili kuja kuwapa shida Watanzania. Mo ametekwa kwa silaha nne na kama (watekaji) walizoea katika nchi zao sio Tanzania."

Amesema watekaji hao pia walijaribu kulichoma moto gari hilo lakini walishindwa na kuamua kulitelekeza.

Sirro alitumia nafasi hiyo kuwaonya watu mbalimbali waliotoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii wakipingana na maelezo aliyoyatoa jana juu ya ulipofikia uchunguzi wa tukio la kutekwa kwa bilionea huyo.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...