TAMADUNI nyingi nchini India mwanamke ndiye anayewajibika kulipa mahari ili kuolewa tofauti na maeneo mengine duniani, ambayo hufahamika suala hilo liko mikononi mwa mume.
Hata hivyo, malipo ya mahari hiyo ambayo hulipwa familia ya mume kutoka kwa familia ya mke nchini India yamepigwa marufuku nchini India tangu mwaka 1961.
Pamoja na marufuku hiyo, vitendo hivyo bado vinaendelezwa katika jamii nyingi kiasi cha kugeuka kama biashara.
Kwa mfano, wanawake wenye sura mbaya au ulemavu hutakiwa kulipa mahari kubwa kwa familia ya kiume ili waweze kuolewa.
Katika kisa kilicho kusudio la makala haya, mume na nduguye wa kambo wamekamatwa baada ya kushukiwa kumuibia figo mwanamke wa mume huyo ili kujilipia mahari, ambayo awali haikuwa imelipwa.
Vyombo vya habari vimeripoti kwamba mumewe mwanamke huyo kutoka Magharibi mwa Bengal alipanga upasuaji wa eneo moja la tumbo lake wakati alipokuwa akiugua uchungu.