Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla leo Jumamosi Agosti 4, 2018 amepata ajali eneo la Magugu mkoani Manyara na kupata majeraha sehemu mbalimbali mwilini.
Katika ajali hiyo ofisa habari wa wizara hiyo, Hamza Temba amefariki dunia.
Mwenyekiti wa jumuiya ya hifadhi ya jamii ya Wanyamapori ya Buruge (WMA), Ramadhan Ismail amesema waziri huyo anapatiwa matibabu katika kituo cha afya Magugu.
Amesema baada ya kupatiwa matibabu katika kituo hicho cha afya, helkopta imefika eneo hilo tayari kwa kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa matibabu zaidi.
Amebainisha kuwa Dk Kigwangalla ana maumivu katika mbavu, kiunoni na hawezi kutembea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Augostino Senga amesema katika gari hilo alikuwepo Dk Kigwangalla, dereva wake, mwandishi wa habari, msaidizi wake na mlinzi.
Amesema hali ya waziri huyo inaendelea vizuri licha ya kuwa ameumia mkono wa kulia, kifua na shingo.
Amebainisha kuwa Dk Kigwangalla, dereva na msaidizi wake wanaendelea kupata matibabu kituo cha afya Magugu huku taratibu zingine za kuwapeleka hospitali kubwa zikiendelea.
Mbunge wa viti maalumu (CCM), Ester Mahawe amefika katika kituo hicho kumjulia hali Dk Kigwangalla na kubainisha kuwa amepata matibabu katika mkono wake wenye majeraha, anaendelea vizuri.
Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amempa pole Dk Kigwangalla na kubainisha kuwa amekwenda kumjulia hali wakati akipita eneo alipopata ajali, akielekea Babati.
"Anaweza kuongea ni uhakika kuwa Mungu atamponya haraka, sala dua na maombi yenu ni muhimu kwa wote waliokutwa na ajali hii mbaya," ameandika Lema.