Thursday, August 2, 2018

Bibi Amchoma Moto Mjukuu Wake wa Miaka Sita Mbeya

Bibi Amchoma Moto Mjukuu Wake wa Miaka Sita Mbeya
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu wawili Judith Amoni Mwansansu(39) ambaye ni bibi wa mtoto na Aive Alex Swalo(17) shangazi yake, kwa kosa la kumfanyia vitendo vya ukatili mtoto, Daines Kefas Mwansasu(06) vya kumuunguza kwa moto na kumpiga.



Kamanda wa Polisi jijini humo, SACP Ulrich Matei, amesema tukio hilo lilifanyika Jumanne July 31, 2018 majira ya saa tatu usiku ambapo siku iliyofuata Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa raia wema kwamba mtoto huyo amejeruhiwa sehemu mbalimbali kwa moto.

"Inadaiwa siku hiyo ya Jumanne, Daines alikuwa ameenda kucheza na rafiki zake na aliporudi nyumbani majira ya jioni shangazi yake alimuadhibu kwa kumchapa na waya wa umeme sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha na maumivu makali mwilini", amesema Kamanda Matei.

Kamanda Matei ameongeza kuwa  August 1, 2018 majira ya asubuhi, watuhumiwa (Shangazi akishirikiana na bibi wa mtoto) waliendelea kumfanyia vitendo vya ukatili mtoto huyo kwa kumuunguza kwa moto sehemu za miguuni na kwenye makalio.

Juni 16, 2018 katika kilele cha siku ya Mtoto wa Afrika, ambayo kitaifa ilifanyika mkoani Arusha na Tanzania ikitajwa kuongoza katika vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kuliko uovu unaofanywa kwenye ujambazi, takwimu zilizowasilishwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , Dk. Faustine Ndugulile, zinaeleza kuwa watoto 41,000 walifanyiwa ukatili kati yao 3,467 kwa kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana.

Lakini pia, Idara ya Ustawi wa Jamii wizarani hapo, ilieleza kuwa asilimia 60 ya ukatili dhidi ya watoto unafanyika nyumbani, asilimia 53 ni shuleni na iliyobaki ni maeneo mengine.

Takwimu zinaonesha watanzania wengi hawajaweza kumlinda mtoto kwa mujibu wa sheria ya mtoto ya mwaka 2009, ambayo imetoa wajibu kwa kila mtu na adhabu kwa anayeshindwa kutekeleza jukumu hilo.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...