Na John Walter -Babati
Wilaya ya Babati mkoani Manyara imetikiswa na mfululizo wa matukio ya vifo vya watu sita ndani ya wiki moja kati ya Aprili 8 hadi 24, mwaka huu wa 2025, vikiwemo vitendo vya mauaji, watu kujinyonga na uporaji.
Katika matukio hayo, matatu yametajwa kuwa ya mauaji ambapo watu watatu wameuawa kwa kuchinjwa katika maeneo ya Gendi Barazani, Kiru Eri na Orngadida.
Aidha, matukio mengine mawili yanahusisha watu waliojinyonga katika kijiji cha Sangaiwe, huku mwingine akijinyonga katika kijiji cha Imbilili.
Katika tukio lingine la kusikitisha, mwili wa dereva wa bodaboda uligundulika katika mtaa wa Negams mjini Babati, ambapo pikipiki yake iliripotiwa kuporwa na watu wasiojulikana.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Manyara, Kija Mkoi, amethibitisha kutokea kwa matukio hayo na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini na kuwakamata wahalifu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, amewasihi wananchi kushirikiana na viongozi wao katika kuwafichua wahalifu badala ya kujichukulia sheria mikononi, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kudumisha amani na usalama katika jamii.
Mkoa wa Manyara unatajwa kushamiri kwa matukio ya ukatili kitaifa na vitendo hivyo vya mauaji vinazidi kudidimiza jitihada za serikali na wadau katika kupunguza au kumaliza kabisa vitendo hivyo vinavyochelewesha Maendeleo katika familia na jamii kwa ujumla.